Famasi ya dawa iliyoko kwenye hospitali ya rufaa ya kanda ya bugando iliyoko
Jengo la huduma za dharura na ajali ambalo linatoa huduma zote zikiwemo za upasuaji
******************
Na.Catherine Sungura-Mwanza
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando(BMC) ipo mbioni kuanzisha taasisi ya moyo ili kuweza kuhudumia wananchi wa kanda ya ziwa.
Akiongea kwenye mkutano wa maofisa habari wa wizara na taasisi wake pamoja na waandishi wa habari jijini hapa mwishoni mwa wiki,Mkurugenzi wa hospitali hiyo Prof. Abel Makubi alisema kuwa wapo mbioni kuanzisha taasisi hiyo itakayokuwa na majengo mawili yenye ghorofa kumi na kumi na tano.
Prof. Makubi alisema kuwa hadi kukamilika kwa majengo hayo wanatarajia kutumia shilingi bilioni 59 .
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kutoa huduma zote za kibingwa na bobezi hapa nchini,hii itapunguzia mzigo serikali na wizara kupeleka wagonjwa nje ya nchi vilevile wananchi wa kanda hii kunufaika na huduma za moyo huku huku”.
Kwa upande wa watumishi Prof. Makubi alisema wameweza kuongeza wataalam wa fani mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wakiwepo wauguzi,madaktari,madaktari bingwa na bobezi na hivyo kufanya kazi ya utoaji huduma katika idara zote bila kuteleleka.
Hata hivyo ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kusomesha madaktari bingwa na bobezi kutoka hospitali hiyo na hivyo kuifanya hospitali hiyo kutoa huduma za kibingwa ikiwemo matatizo ya tumbo,mifupa,koo,pua na ndomo,macho,mfumo wa mkojo,meno,ubongo na mishipa ya fahamu pamoja na matatizo ya akina mama.
“Huduma za upasuaji kiujumla zimeboreka sana katika awamu hii kwa upande wa upasuaji mkubwa wa kawaida pia,upasuaji maalumu wa midomo sungura,kichwa maji na mgongo wazi pamoja na upasuaji wa fistula”.Aliongeza Prof. Makubi
Aidha,aliishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa MOI kwa,mashirikiano ya karibu katika kutoa huduma za kibingwa,za upasuaji katika mikoa mbalimbali ya kanda ya ziwa