Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Adolf Ndunguru akifungua
warsha ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Uasilishaji wa Agenda 2063,
ambapo alisema kuwa Serikali itahakikisha Watanzania wanajua maana ya Agenda
2063 na umuhimu wake wakati wakifungua warsha hiyo Jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. William Mhoja (wa
pili kushoto) akizungumza jambo na Afisa Mwandamizi wa Sera Kamisheni ya
Umoja wa Afrika, Bw. Oitsile Thesunyiwe (wa pili kulia) baada ya kumalizika kwa
warsha ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Uasilishaji wa Agenda 2063,
Jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. William Mhoja (wa
saba kulia), Afisa Mwandamizi wa Sera Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bw. Oitsile
Thesunyiwe (wa sita kulia) pamoja na baadhi ya wadau wa warsha ya Kamisheni ya
Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Uasilishaji wa Agenda 2063 wakiwa katika picha ya
pamoja baada ya warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango Jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
Adolf Ndunguru (katikati), wakifuatilia kwa makini ajenda zinazowasilishwa na wadau
katika warsha ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Uasilishaji wa Agenda
2063 Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango)
*****************
Na. Farida Ramadhani na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Tanzania imejipanga kutekeleza Mpango Mkakati wa Maendeleo kwa nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo kuchochea maendeleo endelevu nchini na kupunguza umaskini kwa wananchi wake.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru, wakati wa warsha ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuhusu Uasilishaji wa Agenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika.
Bw. Ndunguru ameeleza kuwa, Tanzania imejipanga kutengeneza mazingira yatakayowezesha kutekeleza mpango huo nchini kwa kuhakikisha unaingia katika mipango ya maendeleo ya nchi ili kuchochea maendeleo ya huduma za afya, utoaji wa elimu, maendeleo ya viwanda pamoja na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema maendelo sio kwa ajili ya watu wachache hivyo Serikali imejipanga kushirikisha wananchi wote katika kutekeleza mpango mkakati huo kwa kuhakikisha wanaelewa chanzo cha mpango huo pamoja na manufaa yake nchini.
“Tumeamua kuuleta mkakati huu nyumbani ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanajua Agenda 2063 ya maendeleo na umuhimu wake kwao, kila mtanzania ajione ni sehemu ya mpango huo na hakuna atakayeachwa nyuma”, alisisitiza Bw. Ndunguru.
Akizungumzia Mpango Mkakati huo, Kamishna Msaidizi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Wiliam Mhoja, alisema kuwa Agenda 2063 ni Mpango Mkakati wa Maendeleo ya AU, ambao umejiwekea malengo takribani 20 kuhusu ukuaji wa uchumi jumuishi pamoja na maendeleo endelevu.
Alisema kuwa miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri kama reli na barabara ambayo itaunganisha nchi zote za Afrika.
Bw. Mhoja alisema kuwa mpango huo utaanza kuwekwa katika mpango wa maendeleo ya nchi pamoja na kuwajengea wananchi uelewa ikizingatiwa kuwa Taifa lipo katika uandaaji wa mpango wa tatu wa maendeleo.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Sera kutoka Kamisheni ya AU, Bw. Oitsile Thesunyiwe, alisema kuwa Kamisheni hiyo imekuwa ikijenga uelewa wa kuhusu Agenda 2063 kwa nchi Wanachama wa umoja huo ambapo Tanzania ni nchi ya 43 kutembelewa kati ya nchi takribani 55 katika umoja huo.
Alisema katika kutoa uelewa wa agenda hiyo, Kamisheni ya Umoja wa Afrika inafanya mazungumzo na nchi hizo kuhusu namna ya kuhuisha Agenda 2063 katika mipango ya maendeleo ya Taifa na ya kisekta.