Na Mathew Kwembe, Dodoma
Michuano ya netiboli ligi daraja la kwanza imeendelea tena leo katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo katika mchezo wa kusisimua uliochezwa jioni umeshuhudia timu ya netiboli kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ‘TAMISEMI QUEENS’ ikiwachapa maafande wa JKT Makutupora kwa magoli 34-27.
Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa takribani dakika 40 baada ya kundi kubwa la nyuki kuvamia uwanja huo na kusababisha taharuki kwa wachezaji na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo.
Magoli yote ya TAMISEMI QUEENS yalifungwa na mfungaji hodari wa timu hiyo Lilian Jovin, ambaye kutokana na umahiri aliounyesha katika ligi hiyo anatarajiwa kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Kwa matokeo hayo, timu ya TAMISEMI QUEENS ipo nafasi ya tatu baada ya kupata jumla ya pointi 12 katika michezo 8 iliyocheza ambapo timu hiyo ilifanikiwa kushinda michezo 6, na kufungwa michezo miwili.
Wanaoongoza ligi hiyo ni timu tishio ya JKT Mbweni iliyo na pointi 14 baada ya kucheza michezo 7 na kufuatiwa na Jeshi Stars ambao nao wana pointi 14, na nafasi ya tatu na ya nne zikichukuliwa na TAMISEMI QUEENS na Jiji la Arusha, huku timu zote zikiwa na pointi 12 isipokuwa timu ya TAMISEMI QUEENS ikiwazidi jiji la Arusha kwa wingi wa magoli ya kufunga.
Akizungumzia michuano hiyo Kiongozi wa TAMISEMI QUEENS Rose Makange alisema kuwa timu yake ipo vizuri kwani kufikia sasa imeshinda michezo 6 kati ya 8 waliyokwishacheza na akaahidi kufanya vizuri katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya wanaoongoza ligi hiyo JKT Mbweni.
Bi Makange ameongeza kuwa timu yake haiwaogopi timu yoyote na akawataka JKT Mbweni ambao watakutana nayo siku ya jumamosi tarehe 7 septemba, wajiandae kwa kipigo kitakatifu kutoka kwa timu yake.
Hata hivyo kiongozi huyo wa TAMISEMI QUEENS amelalamikia kukiukwa kwa kanuni za uendeshaji wa ligi hiyo kufuatia baadhi ya timu kuchezesha zaidi ya wachezaji watatu wa kutoka nje ya nchi kinyume na kanuni zinazotaka timu hizo kutochezesha zaidi ya wachezaji watatu.
Bi Makange amewataka viongozi wa chama cha mchezo wa pete Tanzania (Chaneta) kutofumbia macho ukiukwaji wa kanuni hizo, na akataka chama hicho kutenda haki kwa kutoa adhabu kwa timu zilizokiuka kwa makusudi kanuni hiyo ili ligi hiyo impate mshindi halali.