*******************
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amesisitiza dhamira ya Serikali katika kulipa
kipaumbele suala la kufanya utafiti, kuwa inalenga kuzitafutia
majibu na ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika
Wizara za Serikali.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini Zanzibar, wakati akipokea
taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi kwa Wizara ya Nchi, Ofisi
ya Makamo wa Pili wa Rais kwa mwaka 2018/2019.
Alisema ni muhimu kwa Idara na taasisi zote za serikali kufanya
utafiti, badala ya jukumu hilo kuiachia Idara ya Mipango, Sera na
Utafiti pekee.
Alisema katika kufanikisha jambo hilo, Idara zinaweza kuwatumia
wataalamu wake na pale wanapokosekana, ni vyema ikatowa
mafunzo kwa wafanyakazi wenye elimu ya kutosha, ili hatimae
waweze kutumika kwa kazi hiyo, na kubainisha kuwa baadhi ya
tafiti hazihitaji fedha nyingi.
Aliwataka viongozi wa Idara za Serikali kujenga mapenzi ya
kufanya tafiti, sambamba na kujenga uwezo wa kitaaluma ili
waweze kutekeleza shughuli hizo kwa ufanisi.
Aidha, aliitaka Wizara kupitia Idara ya Sherehe na Maadhimisho
ya kitaifa kuwasilisha waraka Serikalini, ili kupata muafaka baada
ya kubainika kuwepo kwa baadhi ya Wizara zilizonunua vifaa mbali mbali vya sherehe, ikiwemo mashamiana kwa lengo la kuvikodisha , jambo ambalo kimsingi linapaswa kufanywa na Idara hiyo.
Akigusia mchakato wa serikali kuihamishia mjini Dodoma Idara ya
Uratibu wa shughuli za Serikali iliopo Dar es Salaam, Dk. Shein
alisema eneo la ardhi la ekari 30 ililopatiwa serikali ya Zanzibar
na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni kubwa,
hivyo akasisitiza azma ya Serikali ya kuihamishia Ofisi hiyo
Dodoma, mara baada ya hatua ya ujenzi kukamilika.
Alisema eneo hilo linapaswa kutumika vizuri kwa kuwepo
mipango mizuri ya ujenzi , kuambatana na maelekezo ya
Mainjinia, pamoja na kutoa indhari ya kuhakikisha ardhi hiyo
inabaki salama.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali kupitia vyombo vyake vya
Ulinzi na Usalama imejipanga vyema na vimekuwa vikifanya
juhudi kubwa kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya,hivyo
akabainisha umuhimu wa kuzifanyia kazi taarifa za uhalifu katika
maeneo yote, ikiwemo baharini.
Katika hatua nyengine, Dk Shein aliwakumbusha watendaji wa
Ofisi hiyo, kuwa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kama ilivyo
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, zinahitaji
wafanyakazi wanaoheshimika na kufanya kazi zao kwa misingi
nidhamu, weledi na uwajibikaji.
Alisisistiza haja ya watendaji hao kuondokana na hali ya
kufanyakazi kwa mazoweya, ili kuweza kupata ufanisi katika
malengo wanayojiwekea.
Aidha, alisema utaratibu wa Bango kitita ni wa kilimwengu,
akibainisha uzuri wake, kwa misingi kuwa unawawezesha wafanyakazi kujitathmin kutokana na utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema miongoni mwa mambo yanayoleta ufanisi katika kazi ni
pamoaj na kuwepo kwa maeneo na ofisi nzuri za kufanyia kazi,
jambo ambalo Serikali imekuwa ikiendelea na juhudi za
kuimarisha.
Dk. Shein aliwapongeza watendaji wa Ofisi hiyo kwa juhudi
kubwa wanayofanya katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja
kazi nzuri waliyofanya katika uwasilishaji wa mpango kazi kwa
mwaka 2018/2019.
Nae, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd,
aliwataka watendaji wa Ofisi hiyo kujifunza na kutekeleza kwa
ufanisi yale yote walioelekezwa, kuambatana na shabaha na
malengo waliyojipangia.
Aliwataka watendaji hao kuendelea na mshikamano wao na
kufanya kazi kwa pamoja, akibainisha kuwa ndio siri ya mafanikio
waliyoyapata, mbali na baadhi nyakati kukabiliana na matatizo
mbali mbali.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi
Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Waziri wa Wizara hiyo
Mohamed Aboud, alisema Ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa
katika kipijndi hicho, ikiwemo kuratibu ujenzi wa nyumba ya
makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais unaoendelea kufanyika
katika eneo la Pagali, kisiwani Pemba.
Alisema ujenzi huo unafanyika chini ya kikosi cha KMKM ambapo
hadi kufikia sasa tayari umefikia asilimia 75 ya kazi.
Alisema Ofisi imefanikiwa kuratibu na kuendesha Uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Jang’ombe, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wapiga kura kwa makundi mbali mbali ya kijamii, ikiwemo walimu na wanafunzi wa sekondari na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Zanzibar.
Aidha, alisema Tume ya Uchaguzi imefanikiwa kubadilisha
mfumo wa Uandikishaji na kutengenza mfumo mpya kwa kutumia
wataalamu wa ndani.
Alieleza kuwa ndani ya kipindi hicho, Wizara ilibeba dhima ya
kuwaelimisha wafanyakazi, wanafunzi wa skuli za msingi na
sekondari pamoja na wananchi katika shehiya mbali mbali
Unguja na Pemba juu ya athari ya matumizi ya dawa za kulevya.
Sambamba hilo, alisema Ofisi ilifanikiwa kuteketeza dawa za
kulevya zilizokuwa maeneo ya uhifadhi wa kisheria, jambo
ambalo kwa mara ya mwisho lilifanyika mnamo mwaka 2009.
Waziri Aboud, alieleza kuwa Ofisi ya Baraza la Wawakilishi
imeendelea na shughuli zake za kuratibu mikutano ya Baraza
pamoja na kazi za Kamati za kudumu kwa ufanisi mkubwa.
“Jumla ya mikutano minne ilifanyika, ambapo kutokana na
mikutano hiyo jumla ya miswada mitano ya sheria ilijadiliwa na
kupitishwa na Baraza”, alisema.
Alisema kazi za kamati za kudumu zilifanyika kupitia Wizara zote
za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na mashirika yake.
Aidha, alisema Ofisi ilifanikiwa kuendeleza ujenzi wa Kituo cha
Tiba na marekebisho ya tabia katika hatua ya tatu pamoja na
kutoa mafunzo katika masuala ya UKIMWI, afya ya uzazi na
uzingatiaji wa masuala ya UKIMWI kwa watendaji wa vyuo vya
Mafunzo na Asasi za kiraia.
Katika hatua nyengine, Waziri Aboud alisema Ofisi ilichukuwa
hatua ya kulihami eneo la fukwe huko Msuka ili lisiendelee
kumong’onyoka kutokana na maji ya bahari, kwa kuandaa
utaratibu wa kujenga ukuta maalum utakaogharamiwa na Serikali
ikiwa ni hatua ya muda.
Aidha, Ofisi iliwapatia mafunzo ya kazi na utaratibu wa maisha
wafanyakazi wa Ofisi, ikiwemo mafunzo ya sheria na kanuni za
Utumishi wa Umma, masuala ya Ukimwi na Homa ya Ini, rushwa
na uhujumu uchumi, udhibiti na utunzaji wa kumbu kumbu na siri
za serikali, pamoja na mkataba wa Huduma za umma.
Waziri Aboud, alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo pia
kulijitokeza changamoto mbali mbali, ikiwemo upungufu wa gari
katika baadhi ya Idara, ufinyu wa nafasi katika mamlaka ya
Usimamizi wa Mazingira, Idara ya Mazingira pamoja na Tume ya
Uchaguzi za Wilaya.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa
Rais, Shaaban Seif Mohamed, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa
kuanzisha utaratibu wa kuwasilisha Mpango kazi na kusema una
faida kubwa katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya
Wizara za serikali.