MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
WANAFUNZI wanaohitimu elimu ya msingi wameaswa kuacha kujiingiza katika vitendo visivyo na maadili mema na vishawishi, kwani inasababisha kukatisha ndoto zao kitaaluma pamoja na kushindwa kuendelea elimu ya juu.
Rai hiyo ilitolewa na alhaj Hamisi Nassor kiongozi wa Maimamu Jimbo la Chalinze, aliyemwakilisha Mufti Abuubakar Zuber katika mahafali ya kuwaaga wahitimu wa elimu a msingi katika shule ya Modern, Chalinze ,Bagamoyo mkoani Pwani.
Alisema watoto hao wanapaswa kujua elimu ni ufunguo wa maisha yao hivyo wasikubali kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya ,bangi na kwa watoto wa kike wasikubali kurubuniwa na vishawishi na tamaa zinazosababisha kupata mimba za utotoni.
Nassoro aliwataka wanafunzi hao ,kwenda kuendelea na masomo ya ziada wawapo majumbani wakisubiri matokeo yao kisha kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari.
Nae mkurugenzi wa Kimara Islamic Sheikh Abdul Kiriwe, alieleza, Chalinze Modern School ni tawi la Kimara Islamic Central iliyopo Kimara jijini Dar es Salaam, ambapo kutokana na ufinyu wa eneo wakanunua ardhi katika eneo hilo la Chalinze Mzee na kujenga shule hiyo ya msingi.
“Hapa tulipokuja kununua eneo hili kwa bahati mbaya kuna kipande ni cha majimaji hivyo hatuwezi kukitumia, hapa mbele yetu kuna eneo kubwa la serikali ambalo halitumiki, tunakuomba mgeni rasmi ukatuombee kwa Rais Dkt. John Magufuli tuweze kupatiwa,” alisema Sheikh Kiriwe.
Akizungumzia changamoto na ombi la eneo hilo, alhaj Nassor alieleza atalifikisha kwa Muft Zuberi na kwamba ataongozana nae kwenda kukutana na Rais Dkt. John Magufuli.
Awali mwenyekiti wa KIC ,Twaha Taslima alieleza, shule inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa majengo ya kutosha kuwezesha kuoatikana shule ya sekondari,jengo la maktaba na bwalo la chakula kwa watoto wa kike.
Mwalimu Mkuu Amrani Bakari alisema shule hiyo inafanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kata, wilaya, mkoa na Kitaifa.