KUPATIKANA KWA MTOTO ALIYEIBWA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye JESCA WILSON BUKUKU [25] Mkazi wa Mtaa wa Kagera – Mama John Jijini Mbeya akiwa na mtoto IRETH ISMAIL, mwenye umri wa miezi sita [06] akiwa hai.
Awali tarehe 29 Agosti, 2019 saa 19:30 usiku mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye ELIZABETH MGINA [22] Mkazi wa Soweto ambaye ni mjasiliamali aliripoti kuibwa kwa mtoto wake huyo na mwanamke asiyefahamika baada ya mwanamke huyo kufika sehemu yake ya biashara kama mteja kwa lengo la kununua vitunguu lakini mtuhumiwa alidai hana hela hivyo waende pamoja nyumbani kwake akampe hela kiasi cha shilingi elfu moja.
ELIZABETH MGINA anaeleza baada ya kuongozana pamoja wakiwa njiani mtuhumiwa aliomba amsaidie kumbeba mtoto huyo na baadae alifika kwenye nyumba aliyodai ni nyumbani kwake na kuomba amsubiri kisha kutokomea na mtoto huyo.
Jeshi la Polisi lilianza msako mkali na mnamo tarehe 04 Septemba, 2019 saa 15:00 alasiri huko Kijiji cha Kyukula kilichopo Kata ya Kyimo, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe alikamatwa JESCA WILSON BUKUKU [25] Mkazi wa Mtaa wa Kagera – Mama John Jijini Mbeya akiwa na mtoto huyo. Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
KUFIKISHWA MAHAKAMANI WATUHUMIWA 28 KWA TUHUMA ZA KUHARIBU MALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya tarehe 02 Septemba, 2019 limewafikisha Mahakama ya Wilaya ya Kyela watuhumiwa 15 wote wanaume CC 134/2019 kwa tuhuma za kuharibu mali. Watuhumiwa wengine 13 kati yao wanawake 02 wanatarajia kufikishwa Mahakamani hapo tarehe 05 Septemba, 2019 kwa tuhuma hiyo hiyo.
Awali mnamo tarehe 28.08.2019 saa 15:30 alasiri huko Kijiji cha Mpunguti, Kata ya Mababu, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela kundi la vijana waliamua kujichukulia sheria mkononi kwa kuharibu magari mawili ya serikali yenye namba za usajili STL 2423 mali ya ofisi ya mkuu wa wilaya ambalo lilivunjwa kioo cha mbele na gari namba T.899 BFS mali ya ofisi ya usalama wa taifa Wilaya ya Kyela ambalo lilivunjwa vioo vyote kwa kupigwa mawe.
Chanzo cha tukio ni kufariki ghafla kwa kijana aitwaye RICHARD MWAKAMOGO wakati akicheza mpira kijijini hapo tarehe 27.08.2019 saa 17:00 jioni hivyo kufuatia tukio hilo kundi la vijana waliituhumu familia ya marehemu kuhusika na kifo hicho na kuilazimisha familia hiyo imfufue.
Kutokana na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kyela ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya CLAUDIA KITA ilifika eneo hilo kwa ajili ya kutatua mgogoro huo na ndipo vijana hao walianza kurusha mawe na kusababisha uharibifu wa mali yakiwemo magari ya serikali. Awali jumla ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa 40.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WANAOJIHUSISHA NA UVUNJAJI NA WIZI WA MALI KATIKA MADUKA YA WAFANYABIASHARA.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na operesheni ya kukamata watuhumiwa waliohusika katika tukio la kuharibu mali ambapo mnamo tarehe 02 Septemba, 2019 alikamatwa JABIR LWITIKO [22] Mkazi wa Ipinda Wilaya ya Kyela ambaye ameunda kikundi cha uhalifu kinachopita kwenye maduka ya watu na kuvunja na kuiba mali mbalimbali.
Baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri kuhusika katika matukio ya kuvunja maduka na kuiba na kuwataja washirika wenzake ambapo katika operesheni ya kuwasaka alikamatwa mwanamke mmoja aitwaye TUKUPASYE KASINGA [30] Mkazi wa Ipinda akiwa na mali mbalimbali zinazodaiwa kuwa za wizi ambazo ni:-
- Kret tupu nne za soda,
- Dawa za meno boksi mbili aina ya Alovera,
- Dumu tatu zenye mafuta ya mawese,
- Soda nane aina ya Sprite [take away]
- Rasta bunda tatu,
- Nywele bandia aina ya Weaving bunda moja,
- Vitenge vipya doti mbili,
- Kuku watatu
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia waganga wawili wa kienyeji 1. GODWIN ANDEMBWISYE [64] na NCHELILE MWANGONDA [71] wote wakazi wa Kijiji cha Mpuguti kwa tuhuma za kushawishi watu kufanya fujo Kijiji cha Mpuguti kwa kuwaaminisha kuwa marehemu RICHARD MWAKAMOGO [26] hajafa bali mama yake mzazi amemfanya msukule hivyo kuitaka familia ifukue na kupekua nyumba yake.
Aidha baada ya kupekua nyumbani kwa watuhumiwa ilikupatikana ngozi ya chatu na dawa mbalimbali za kienyeji. Watuhumiwa hawana leseni inayowaruhusu kufanya kazi ya uganga. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
TAARIFA YA KIFO.
Mnamo tarehe 03.09.2019 saa 14:30 mchana huko Kijiji cha Igomelo katika Mto Mbarali uliopo Kata na Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Mtoto DANIEL RICHARD @ MWAKYANGA [13] mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Igomelo na mkazi wa Igomelo alikutwa akiwa amefariki dunia baada ya kuzama kwenye maji ya mto Mbarali wakati alipokuwa anaogelea.
Marehemu aliondoka nyumbani kwao tarehe 02.09.2019 saa 17:00 jioni akidai anaenda masomo ya ziada “tution” ndipo hakuonekana tena hadi alipokutwa akiwa amefariki dunia katika mto huo. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na daktari. Chanzo cha kifo ni kukosa hewa. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mbarali. Upelelezi unaendelea.
OPERESHENI MBALIMBALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na operesheni mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu katika maeneo mbalimbali kwa kufanya doria na misako yenye tija katika maeneo yote ili kuhakikisha mkoa wetu unakuwa salama wakati wote.
Aidha tunaendelea na operesheni za kuzuia na kudhibiti makosa mbalimbali ya barabarani kwa kukamata madereva na wote wanaokiuka sheria na taratibu za usalama barabarani wakiwemo madereva wa bajaji na pikipiki @ bodaboda. Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kitengo cha Polisi Jamii na elimu kwa umma tunaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wote wa barabara ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2019.
Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama wakati wote wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambao umewasili tarehe 03.09.2019 hapa Mbeya na utakimbizwa katika Wilaya zote tano [05] na halmashauri zote saba [07] za Mkoa wa Mbeya hadi tarehe 09.09.2019. Hivyo ni wito wetu Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya kwa wananchi wote kuhakikisha wanashiriki katika mbio hizo kwa amani na utulivu bila kuwepo kwa vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani na kuwa tayari kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na uvunjifu wa amani kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za haraka zaidi.