**********
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe, Ally Hapi amewataka vijana nchini kutumia muda wao kufanya kazi zenye tija kiuchumi badala ya kukesha kwenye mitandao ya kijamii wakituma na kubishana mambo yasiyo na tija kwao na kwa taifa.
Mhe, Hapi ameyasema hayo leo wakati akifungua kongamano la fursa za kiuchumi kwa vijana zaidi ya 500 wa Wilaya ya Kilolo.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe, Rais Dkt John Magufuli, imejipanga kuwawezesha wananchi kiuchumi na kwa upande wa vijana ,wanawake na walemavu kuna fedha za mikopo kupitia Halmashauri inayotolewa ambako kwa Mkoa wa Iringa takribani bilioni 1.2 imetolewa kwa mwaka 2018/2019. RC.Hapi amewataka vijana kuchangamkia fursa za mikopo hiyo badala ya kupoteza muda kwa mambo ya hovyo mitandaoni na vijiweni.
”Taifa letu linawategemea vijana, nyinyi ndio nguzo ya uchumi wa taifa. Hamna budi kutumia muda wenu vizuri kwa mambo yenye tija kwenu kiuchumi…” Alisema RC.Hapi.
Aidha, RC.Hapi amezitaka halmashauri za Iringa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wanaopewa mikopo ili wawe na uwezo wa kufanya biashara kwa ufanisi na kurejesha mikopo hiyo.
“Nazitaka halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kutoa kipaumbele kwa wale waliopewa mafunzo ya ujasiriamali kwani hawa mtakua na hakika watatumia mikopo kwa malengo sahihi.” alisema Mhe Hapi.
Hapi amezitaja fursa za kiuchumi kwa vijana kuwa zipo nyingi zikiwemo za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ambapo soko kubwa la maziwa lipo kwenye kiwanda cha ASAS Iringa ambacho kina uhitaji mkubwa wa maziwa huku maziwa wanayopata yakiwa hayatoshelezi mahitaji ya kiwanda.
Hata hivyo RC Hapi alisema mkoa wa Iringa unajiandaa kwa kulitumia shamba la mitamba la Sao Hill Mufindi kwa kuzalisha na kukopesha Ng’ombe kwa makundi mbalimbali ili kuwezesha kukuza sekta ya maziwa kama chanzo cha kipato.