Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhe. Selemani Jafo akifungu Mkutano wa Chama cha Madaktari wa
Kikristo Tanzania uliofanyika St. Gasper Jijini Dodoma.
Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania Dr. Bwire
Chirangi akiwasilisha risala kwa mgeni rasmi wakati wa kufunga
kikao cha madaktari hao wa Taasisi za Dini zinazotoa huduma za
Afya Tanzania.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhe. Selemani Jafo(kulia) akiwa na Mkurugenzi wa CSSC Mr.
Maduku wakati wa kufunga Mkutano wa Chama cha Madaktari wa
Kikristo Tanzania.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Chama cha Madaktari wa
Kikristo Tanzania wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa
kufunga kikao cha madaktari hao wa Taasisi za Dini zinazotoa
huduma za Afya Tanzania.
Baadhi ya mshiriki wa Mkutano wa Chama cha Madaktari wa Kikristo
Tanzania akifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa kufunga kikao
cha madaktari hao wa Taasisi za Dini zinazotoa huduma za Afya
Tanzania.
**************.
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Selemani Jafo amewataka viongozi wa dini Nchini kote kuendelea
kuliombea Taifa hasa wakati huu ambao miradi mikubwa ya maendeleo
inatekelezwa.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa 82 wa Chama
cha Madaktari wa Kikristo Tanzania unaofanyika chini ya Taasisi ya
Huduma ya Kijamii za Kikristo(CSSC) katika ukumbi wa St. Gasper Jijini
Dodoma.
Waziri Jafo amesema “Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi
mikubwa ambayo haijawahi kutokea tangu Uhuru, kila unapopita unaona
ujenzi wa miundombinu ya barabara inaendelea, halkadhalika ujenzi wa reli
ya kisasa (SGR), huku mradi wa ufuaji umeme wa mto Rufiji unatekelezwa
hatuna budi kuendelea kumuombea Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe
Magufuli azidi kuwa na afya njema na aweze kusimamia miradi hii hadi
ukamilifu wake”.
Tunashukuru Mungu leo hii Mahakamu Kuu ya Gauteng, Africa Kusini
imetoa hukumu na kuamuru ndege yetu ya Air Tanzania iliyokuwa
inashikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi hizi
ni habari njema sana kwetu na haya ni matunda ya kufanya vitu kwa nia
njema na dhamira ya dhati ya kuwainua watanzania tusiache kuomba kwa
ajili ya Taifa hili aliongeza Jafo.
Wakati huo huo Waziri Jafo aliziagiza Halmashauri zenye Hospitali Teule
(DDH) kuhakikisha wanafanya vikao na Taasisi za kidini zenye
makubaliano ya uendeshaji wa Hospital hizo.
“Hizi tabia za Halmashauri kusema hawana hela za vikao sjui viburudisho
zisikwamishe ufanyikaji wa vikao, kutaneni hata saa nane mchana mpaka
kumi jioni cha msingi mjadiliane changamoto zinazokabili hospitali hizo na
kuzitaftia njia ya kuzitatua kwa pamoja” alisema Jafo.
Kuna changamoto ndogondogo ambazo zinaweza kutatuliwa kwa
mashauriano tu lakini unapoziacha kwa muda mrefu zinakuwa tatizo
kubwa, mkiwa mnakutana ni vizuri katika uboreshaji wa huduma za Afya
kwenye Halmashauri husika aliongeza Jafo.
“Taasisi za Dini mnafanya kazi kubwa sana katika Sekta ya Afya na kwa
muda mrefu mmekuwa mkimiliki Hospital takribani 105 na Serikali tulikuwa
na Hospital 77 tu kabla hatujaanza ujenzi wa Hospital za Wilaya 67.
Mmekuwa msaada katika kuwafikia wananchi ambao Serikali ilikua bado
haijajenga Hospital niwapongeze kwa kuhakikisha huduma za Afya
zinapatikana karibu na wananchi na kwa haraka hakika mmewasaidia
watanzania wetu kupata huduma bora za Afya na mmeboresha afya zao
Alisema Jafo.
Halkadhalika Waziri Jafo aliweka wazi mpango wa Serikali kukamilisha
mchakato wa kuajiri Watumishi wa Afya takribani 400 ambao kwa kiasi
flani wataenda kupunguza uhaba wa watumishi wa Afya katika Vituo vya
kiutolea huduma za Afya.
“Ninafahamu fika tatizo la uhaba wa watumishi katika hospital nyingi
Serikali tunalifahamu hilo na tumechukua hatua za makusudi za kutangaza
ajira za Afya na sasa tunakamilisha mchakato wa ajira hizo na muda si
mrefu mtaanza kuwapokea kwenye baadhi ya Hospital ambao wataongeza
nguvu katika utoaji wa huduma za Afya Nchini” Alisema Jafo.
Akizungumza katika Kikao hicho Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo
Tanzania Dr. Bwire Chirangi alitaja changamoto zinazowakabili ni pamoja
na kukosa vikao vya mashauriano, uhaba wa watumishi wa Afya pamoja
na miundombinu duni ya kuzifikia huduma za Afya.
Aidha Dr. Chirangi alieleza kuwa Chama hiki kimeanza mwaka 1937 na
kinawakutanisha pamoja wataalamu wote wa Afya wanaohudumu katika Hospital za Dini na wamekuwa wakikutana kila mwaka kujadili changamoto na mafanikio mbalimbali ya huduma za Afya zinazotolewa na Taasisi za Dini ya Kikristo.