Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika kikao cha pamoja na Wenyeviti wa Mitaa na vitongoji wakijadili masuala mbalimbali ya sekta ya afya leo, katika kijiji cha Mkoyo, kata ya Hombolo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akikagua kitabu cha kuingizia dawa katika Zahanati ya Ipala kilichopo, katika kijiji cha cha Mwinyi , Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akikagua chumba cha dawa katika Zahanati ya Ipala iliyopo, katika kijiji cha cha Mwinyi , Halmashauri ya Jiji la Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akionyesha mashine ya POSS inayotumika kwa ajili ya kukusanyia mapato katika Zahanati ya Ihumwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma
……………………
Na. Angela Msimbira HOMBOLO
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima amewaagiza watumishi wa Sekta ya afya ngazi ya Msingi kuhakikisha wanashirikisha Viongozi wa Mitaa, Vijiji na Kata mipango yote ya afya inayohitaji ushirikishwaji wa wananchi.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo wakati alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea vituo vya kutolea huduma kwa lengo la kujionea maendeleo ya utoaji wa huduma za afya kwa jamii pamoja na matayarisho ya vituo hivyo katika kushiriki huduma za afya ya kinga katika kijiji cha Mkoyo, Kata ya Hombolo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanawashirikisha viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali ili, somo la afya liweze kuwafikia wananchi wa makundi yote kokote waliko kwa kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga uelewa na kufanyakazi kwa pamoja.
Dkt. Gwajima amefafanua kuwa, watumishi wa sekta ya afya ngazi ya msingi wanatakiwa kuwasiliana na Viongozi wa ngazi zote kuanzia Kitongoji, Mtaa, Kijiji, Kata hadi ngazi ya juu katika Halmashauri na Mkoa kuhusu masuala yote ya afya yanayohitaji ushiriki wa wananchi ili kuwezesha viongozi hawa kuibeba vizuri ajenda ya afya na kuwaelewesha wananchi.
Amewahimiza watumishi wa sekta ya afya ngazi ya msingi kuhakikisha nao wanagonga milango ya viongozi hawa na kuwapa ajenda za afya zinazohitaji ushiriki wa wananchi kwa kuwa viongozi hao ndiyo wenye dhamana ya kwanza kabisa ya uongozi wa wananchi hivyo, ni fursa kubwa endapo tutaendelea kushirikiana nao kwa karibu zaidi.
“kufanya kazi pamoja na viongozi wa serikali katika ngazi ya kitongoji, mtaa, kijiji, kata na ngazi zingine zote za uongozi wa serikali na jamii kutasaidia kuharakisha uelewa wa wananchi juu ya ajenda za afya na juhudi za serikali na hatimaye, kuwezesha wananchi wengi zaidi kushiriki shughuli za kijamii zinazolenga kuboresha afya ya jamii kwa ujumla ili, kujenga taifa lenye afya bora kwa gharama nafuu kabisa maana kinga ni bora kuliko tiba” Amesema Dkt. Gwajima
Amesema kuwa, viongozi wa ngazi ya kitongoji, mtaa, kijiji, kata na ngazi zingine zote wakielewa vizuri sera, miongozo na mipango mbalimbali ya serikali kuhusu afya ya jamii wataendelea kuwa mabalozi na wasimamizi wazuri wa kufikisha ujumbe kwa jamii kwa haraka na kuwezesha kuhamasisha jamii husika kushiriki katika masuala ya afya yanayohitaji wananchi.
Dkt. Gwajima amewashukuru viongozi mbalimbali wa serikali na jamii ngazi zote kwa ushirikiano wao wakati wote katika kuibeba ajenda ya afya na kufanikisha mambo mengi ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya unaoendelea nchi nzima na masuala yote ya elimu ya afya kwa jamii na kuhamasisha wananchi kupata huduma za afya ya kinga.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoyo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma Bw. Henry Kubesi amesema kuwa, yeye na uongozi wote wa Kijiji hicho wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha Uongozi wa Ngazi ya Msingi unatambuliwa, unaheshimiwa na unashirikishwa katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Amesema kuwa, ngazi ya msingi ndio nguzo muhimu katika jamii kwa kuwa wao ndio wanawafikia wananchi kiurahisi zaidi hivyo, tunaishukuru Serikali kwa kulitambua hilo ili kuweza kuongea lugha moja ya kuleta maendeleo kwa jamii. Aidha, Bw. Kubesi ameahidi kuwa yeye akipewa ajenda ya afya huwa anahakikisha mara moja anaanza utekelezaji kwa kuwashirikisha Wenyeviti wa Vitongoji vyote 8 vya Kijiji chake ili waelewe na kupeleka ujumbe husika kwa wananchi.
Naye mhamasishaji wa afya ngazi ya jamii Bi. Anastazia Konyanza amesema kuwa yeye ni mtaalamu anayehusika na eneo la uelimishaji na uhamishaji wa wananchi hivyo, atashirikiana na wataalamu wengine wote kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii yote ya Kijiji cha Mkoyo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhusu masuala yote muhimu ya afya kama ambavyo wamekuwa wakifanya na kupata ufanisi mkubwa ikiwemo kwenye eneo la Bima ya Afya ya Jamii.
Aidha katika ziara hiyo Dkt. Dorothy Gwajima aliambatana na wataalam wa afya kutoka Wizara, Mikoa na Halmshauri ya Jiji la Dodoma.