Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Nd. Cosmas Kimario (kushoto), akikabidhi hundi ya shilingi milioni 500 kwa Rais wa TFF, Nd. Wallace Karia, kwa ajili ya udhamini wa Ligi kuu Tanzania Bara. KCB imeendeleza udhamini wa ligi hiyo kwa msimu wa 2019/20 ikiwa msimu wa tatu mfululizo. Wanaoshuhudia, (watatu kulia) Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya KCB Tanzania, Nd. John Ulanga, (Mkuu wa Idara ya Masoko wa Benki hiyo Bi. Christine Manyeye na Mwanasheria Mkuu waBenki ya KCB , Bi. Anthonia Kilama hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Nd. Cosmas Kimario (wa tatu kushoto), Pamoja na Rais wa TFF, Nd. Wallace Karia, wakionyesha hundi ya shilingi milioni 500 iliyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya udhamini wa Ligi kuu Tanzania Bara. Benki ya KCB imeendeleza udhamini wa ligi hiyo kwa msimu wa 2019/20 ikiwa msimu wa tatu mfululizo. (watatukulia) ni Mwenyekiti wa Bodi Benki ya KCB Tanzania, Nd. John Ulanga, wengine ni viongozi kutoka TFF na KCB.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Nd. Cosmas Kimario (wa tatu kushoto), Pamoja na Rais wa TFF, Nd. Wallace Karia, wakionyesha mkataba wa udhamini wa Ligi kuu Tanzania Bara baada ya kutiliana saini leo jijini Dar es Salaam. Benki ya KCB imeendeleza udhamini wa ligi hiyo kwa msimu wa 2019/20 ikiwa msimu wa tatu mfululizo. (watatukulia) ni Mwenyekiti wa Bodi Benki ya KCB Tanzania, Nd. John Ulanga, wengine ni viongozi kutoka TFF na KCB.
……………….
Benki ya KCB Tanzania imengia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kuwa mdhamini mwenza wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara kwa msimu wa 2019/2020. Mkataba huo wenye thamani ya shilingi za Kitanzania 420,000,000 kabla ya kodi, ulitiwa saini leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Nd. Cosmas Kimario na Rais wa TFF Nd. Wallace Karia katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Benki ya KCB Tanzania ilidhamini ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu wa 2017/18 kwa thamani ya shilingi za Kitanzania 325,000,000 na kuongeza udhamini kwa msimu wa 2018/19 kufikia shilingi za Kitanzania 420,000,000. Mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa udhamini wa misimu iliyopita ndiyo yameivutia Benki ya KCB Tanzania kuendeleza udhamini huo kwa kiasi cha shilingi za Kitanzania 420,000,000 kupelekea jumla ya udhamini ndani misimu mitatu kuwa shilingi za Kitanzania 1.165bn.
Hafla ya kutia saini makubaliano hayo imehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya KCB Tanzania, Nd. John Ulanga, Katibu Mkuu TFF, Nd. Kidao Wilfred, Mwenyekiti wa bodi ya Ligi Kuu, Nd. Steven Mnguto na Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Nd. Boniface Wambura, Pamoja na Wakurugenzi wa Bodi na wafanyakazi Benki ya KCB Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusainiwa mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Nd. Cosmas Kimario alisema kwamba pamoja na dhamira ya benki hiyo kurudisha kwa jamii, udhamini huo pia ni fursa kubwa kwa Benki ya KCB kuwekeza kwenye sekta yenye kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa kukuza ajira na vipaji vya vijana wa Kitanzania.
Zaidi ya kutengeneza ajira kwenye soka, Benki hiyo imewekeza kwenye programu ya KCB 2jiajiri ambayo hadi sasa imetoa mafunzo ya uweledi wa biashara kwa wanawake 256 na vijana 100 kuanzia mwezi Oktoba. “Matarajio ya benki yetu ni kuona Watanzania wengi zaidi wanapata ajira kupitia sekta mbali mbali tunazozigusa.” Alisema Nd. Kimario.
“Sisi Benki ya KCB, mbali na biashara tunatimiza wajibu wetu katika jamii inayotuzunguka kwa kuiunga mkono serikali yetu kupinga umasikini nchini. Hivyo pia tunasaidia jamii hitaji kupitia sekta za: elimu, afya, mazingira, wajasiriamali, watoto waishio katika mazingira magumu.” Aliongeza Nd. Kimario
Rais wa TFF, Nd. Wallace Karia aliishukuru Benki ya KCB Tanzania kwa kuidhamini Ligi kuu Tanzania Bara jambo ambalo alisema litasaidia kufanikisha msimu huu wa ligi kuu 2019/20. Pia alizitaka taasisi zingine na watu binafsi kuiga mfano huo kuweza kutoa michango ya hali na mali ili kukuza maendeleo ya soka kwa timu za ligi kuu.
Kuhusu Benki ya KCB
Benki ya KCB ni benki kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati iliyoanzishwa mwaka 1896 kisiwani Zanzibar. Toka hapo benki imekua na kuenea katika nchi za Tanzania, Kenya Sudani ya Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi na Ethiopia. Leo hii ina mtandao mkubwa zaidi
katika kanda hii ikiwa na matawi 262, mashine za kutolea fedha (ATM) 962, na wakala 15,000 wanaotoa huduma za benki masaa 24 siku saba za wiki Afrika Mashariki.
Benki ya KCB imesajiliwa katika soko la hisa la Nairobi, Dar es Salaam, Uganda na Rwanda. KCB Bank Group pia linamiliki kampuni ya bima ya KCB, KCB Capital na KCB Foundation. Nchini Tanzania, KCB ilifungua milango yake mwaka 1997 na toka hapo imekuwa mdau mkubwa katika kukuza sekta ya fedha nchini. Kwa sasa benki ina matawi 14 Tanzania bara na visiwani Zanzibar. Matawi hayo ni Samora, Mlimani, Uhuru, Msimbazi, Lumumba, Buguruni, Oysterbay, Mbagala jijini Dar es Salaam; Moshi, Zanzibar, Arusha Main na TFA, Mwanza na Morogoro.
Benki ya KCB Tanzania ni mlipa kodi mzuri, mwajiri wa watanzania zaidi ya 300, inafundisha wafanyakazi wake weledi wa kikazi na pia pale inapotokea nafasi inapeleka wafanyakazi katika soko la Afrika Mashariki.