NJOMBE
Baada ya wakazi wa kijiji cha Lole kata ya Ikuna wilayani Njombe kumtupia lawama mkandarasi wa kampuni ya GV Mufindi Power LTD kwa kusuasua katika usambazaji wa umeme wa REA kijijini hapo , Waziri wa nishati Dr Medard Kalemani ameonyesha kukasilishwa na hali hiyo na kumpa siku 20 mkandarasi huyo kuhakikisha anawasha umeme katika vitongoji 7 kati ya 8 vya kijiji hicho ambavyo vipo kwenye mpango na havijafikishiwa huduma hiyo hadi sasa.
Dr Kalemani ametoa agizo hilo baada ya kuwasha umeme katika taasisi ya dini kijijini hapo na kujionea jinsi mkandarasi wa kampuni hiyo anavyokwamisha jitihada za serikali na matakwa ya wananchi katika kuipata huduma ya umeme na kudai kwamba endapo mkandarasi atashindwa kuwasha umeme katika muda aliotoa hatasita kumchukulia hatua mkandarasi wa kampuni ya Mufindi Power na meneja wa TANESCO mkoa wa Njomb.
Mbali na onyo hilo waziri Kalemani amezitaka halmashauri kote nchini kulipia gharama za kuingiza umeme katika taasisi za umma ili wananchi waweze kupata huduma hiyo.
Omega Ngoda,Reymond Michael na Mario Mgaviwa, ni baadhi ya wakazi kijiji cha Lole na Ninga wanasema vijiji vyao vimekuwa na maendeleo ya kusuasua kwasababu ya kukosa nishati ya umeme na kwamba ujio wa huduma hiyo utawafanya kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Licha ya kasi ya mkandarasi kulalamikiwa lakini imedaiwa kwamba watu wengi wapo kwenye hatari ya kuikosa huduma hiyo kwakuwa lamani ya mkandarasi inaonyesha kupita katika maeneo machache ya vijiji vilivyopo katika mpango kama ambavyo diwani wa kata ya Ikuna Paul Kinyamagoha ameeleza mbele ya waziri.
Waziri wa nishati yupo mkoani Njombe kwa ziara ya siku mbili ambapo katika siku ya kwanza amewasha umeme katika taasisi za umma katika kijiji cha Lole na Ninga