Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akiwa na Mbunge wa Mbulu vijijini Mhe. Flatei Gregory Massay na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Bw. Chelestino Mofuga pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati Mhandisi Iddy Msuya wakielekea kukagua mradi wa Tumati uliopo Mbulu vijijini.
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akipata maelezo ya mradi wa Arri Harsha kutoka kwa Mhandisi Maji wa Halmashauri ya Mbulu Philemon Kamar.
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) hayupo pichani.
……………….
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amefanya ziara ya kukagua miradi ya maji yenye changamoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
Waziri Mbarawa amefanya ziara hiyo ili kubaini changamoto zilizopo katika miradi ya maji ili serikali iweze kutafuta ufumbuzi wa haraka na wananchi wa Mbulu waweze kupata majisafi na salama na kutekeleza azma ya kumtua mama ndoo kichwani.
Waziri Mbarawa amesema changamoto kubwa iliyokuwepo ni kuwa wakandarasi wanaopewa kazi hizo za kutekeleza miradi, wanaweka gharama kubwa za ujenzi na kujenga miradi chini ya viwango.
Mhe. Mbarawa amesema kwa muda mrefu Serikali imekuwa inalipa gharama kubwa za kujenga miradi ya maji nchini kutokana na ubabaishaji wa wakandarasi wa kuweka gharama kubwa, kujenga miradi isiyokuwa na ubora na miradi kutokamilika kwa wakati hivyo kuwafanya wananchi wakose majisafi na salama.
“Kuanzia sasa Serikali imekuja na utaratibu mwingine wa kuwatumia wataalam wake wa ndani na Mamlaka za Maji za eneo husika katika utekelezaji wa miradi ya maji ili kupunguza gharama kubwa zilizokuwa zinawekwa na wakandarasi”, Prof. Mbarawa amesema
Miradi iliyokaguliwa ni mradi wa maji wa vijiji vya Mongahay, Tumati, mradi wa maji wa vijiji vya Arri, Yaeda Ampa, Haseng, Harsha Bashay na Yaeda. Mhe. Mbarawa ameahidi kupeleka kiasi cha fedha Tsh. 150 milioni kwa mradi wa Tumati na Tsh. 300 milioni kwa mradi wa Arri Harsha ambazo zimeshafika katika Mamlaka ya Maji Babati kwa ajili ya kuanza kazi za kukamilisha kazi zilizobaki.
Mhe. Waziri Mbarawa akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mbulu na kusikiliza kero zao amewaahidi kwamba kero zao zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha wanapata majisafi na salama.
Waziri Mbarawa amewataka wananchi wa Mbulu kutunza miundombinu ya miradi ya maji na kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.