Dr. Pepretua Kalimasi Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Nje na Ushirikishwaji wa Jamii (DELCE), akifungua mafunzo ya Maafisa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI – Babati na Arusha) mkoani Morogoro. Kushoto ni Dr. Daudi Pascal Ndaki, Mratibu wa mafunzo.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo maalumu ya Uwekezaji Mkakati wakisikiliza kwa makini mafunzo yanayoendelea chuoni Mzumbe Morogoro.
Mkufunzi Mkuu wa mafunzo ya maafisa toka TAMISEMI Dr. Nelson Ngilangwa akijitambulisha kwa washiriki (hawamo pichani). Kushoto ni Dr. Dr. Pepretua Kalimasi.
Baadhi ya Washiriki wakiwa katika majadiliano ya vikundi na wakufunzi wao.
Dr. Daudi Pascal Ndaki akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya Uwekezaji Mkakakati yanayoendelea Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro.
………………….
Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Nje na Ushirikishwaji wa Jamii (DELCE); wanaendesha mafunzo mahsusi kwa Maafisa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa Babati na Arusha kuhusu namna bora ya kuandaa Uwekezaji Mkakati wenye lengo la kuongeza utendaji wenye tija katika kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Akizungunza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo; Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo Dr. Perpetua Kalimasi, amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimejizatiti katika utoaji wa mafunzo bora kuendana na mahitaji ya wadau. Kupitia wataalamu wake wa ndani wameweza kubuni kozi mbalimbali za muda mfupi kuwezesha kuwajengea uwezo na kuwapa ujuzi wataalamu katika sekta mbali mbali ili kuhakikisha malengo ya jumla katika Serikali na Sekta binafsi yanafikiwa.
“ Kama Chuo chenye dhamana ya kutoa Elimu bora kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Nje na Ushirikishwaji wa Jamii; tumebuni kozi nyingi fupi fupi kupitia wataalamu wetu kuweza kufundisha makundi mbalimbali ya watumishi na jamii kwa ujumla ili kuwawezesha kuleta ufanisi na kufikia malengo kulingana na mipango ya kiutendaji waliyojiwekea; hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza katika Uchumi wa Viwanda” alisema
Aidha amewataka washiriki kutumia vema muda wa mafunzo waliojipangia kuhakikisha wanajifunza na kupata ujuzi katika masuala yanayohusu “Uwekezaji Mkakati” ili mafunzo hayo yawawezeshe kuleta mapinduzi katika shughuli wanazozisimia huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa wadau mbali mbali nchini.
Naye mratibu wa mafunzo hayo Dr. Daudi Pascal Ndaki amesema mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha wataalamu hao wanapata mafunzo ya nadharia na vitendo kupitia wataalamu wabobevu na kwamba washiriki watakuwa na fursa nzuri ya kubadilishana uzoefu na kutatua kwa pamoja changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika maeneo yao ya kazi.
Aidha mafunzo hayo yatahusisha mada mbalimbali zinazohusu Uwekezaji Mkakati, mbinu na mikakati ya kuainisha maeneo ya uwekezaji hususani ile inayohusu utatuzi wa matatizo ya jamii na namna ya kuandika miradi inayoweza kupata ufadhili wa ndani na nje. Matokeo ya mafunzo hayo ni kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuandika miradi ya maendeleo na uwezo wa kutafuta fedha za kuanzisha na kuendesha miradi ya maendeleo katika maeneo yao ya kiutendaji.