JAJI MKUU WA TANZANIA MHE. PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA (KUSHOTO) AKIMKABIDHI MKUU WA WILAYA YA MUFINDI MHE. JAMHURI WILLIAM KITABU CHA MPANGO WA MIAKA MITANO WA UJENZI WA MAJENGO YA MAHAKAMA YA TANZANIA ALIPOMTEMBELEA OFISINI KWAKE AKIWA KATIKA ZIARA YA KIKAZI MKOANI IRINGA.
JAJI MKUU WA TANZANIA MHE. PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA MKUU WA WILAYA YA MUFINDI MHE. JAMHURI WILLIAM (WA PILI KULIA) PAMOJA NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA YA MUFINDI ALIPOMTEMBELEA OFISINI KWAKE AKIWA KATIKA ZIARA YA KIKAZI MKOANI IRINGA
JAJI MKUU WA TANZANIA MHE. PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA WATUMISHI WA MAHAKAMA YA WILAYA YA MUFINDI BAADA YA KUZUNGUMZA NAO ALIPOTEMBELEA MAHAKAMA YA WILAYA YA MUFINDI KUKAGUA SHUGHULI ZA MAHAKAMA AKIWA KATIKA ZIARA YA KIKAZI MKOANI IRINGA
Lydia Churi-Mahakama Iringa
Mahakimu wametakiwa kusimamia uendeshaji wa mashauri na kuzuia maahirisho
ya mara kwa mara ya kesi bila ya sababu za msingi kwa lengo la kuhakikisha kesi
zinamalizika kwa wakati Mahakamani.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema hayo wakati wa
kikao cha majumuisho mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku tano katika
mikoa ya Iringa na Njombe aliyoifanya kwa lengo la kukagua shughuli za
Mahakama pamoja na kubainisha kwa wadau changamoto zilizoibuliwa wakati wa
kikao cha Mahakama ya Rufani kilichomalizika leo mjini Iringa.
Jaji Mkuu amewata Mahakimu kutokubali kuahirisha mashauri kwa muda mrefu
kwa ajili ya kuandaa maamuzi madogo yanayotokana na pingamizi ambazo nyingi
hutumiwa vibaya kwa lengo la kuchelewesha mashauri.
“Maafisa wote wa Mahakama ni jukumu lenu pia kuzipa nguvu za kimahakama
vifungu vya sheria zinazolinda haki ya Mwananchi aliye mahabusu kwa
kuhakikisha hakuna mwananchi atashikiliwa bila kufikishwa mahakamani ndani ya
siku zilizowekwa na sheria”, alisema.
Alitoa rai kwa Mahakimu kutokuwa wepesi kukubali hoja za waendesha mashitaka
za kusema kuwa upelelezi bado unaendelea bila ya kufafanua ni kitu gani katika
upelelezi bado kinatafutwa na ni kwa muda gani.
“Ni umakini wa Mahakama ndiyo utahakikisha kuwa shughuli za upelelezi
haziwanyimi wananchi haki yao ya kikatiba ya kutochelewesha haki yao ya
kusikilizwa kesi dhidi yao bila sababu za kimsingi,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Akizungumzia dhamana, Jaji Mkuu amesema ni wajibu wa Mahakama kutoa
dhamana kwa makosa yenye dhamana kwa kuwa Mahakama ni msimamizi wa
haki ya kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu huru.
Alivitaja vigezo vya kutumiwa katika kutoa dhamana kuwa ni pamoja na
vitambulisho vya Taifa, na vitambulisho vinavyokubalika. Aliongeza kuwa
Mahakama pia ziwaruhusu washtakiwa kujidhamini wenyewe pale Hakimu
anapojiridhisha na utambulisho wao kuwa watahudhuria mahakamani.
“Mashauri ambayo washtakiwa wamekosa dhamana yasikilizwe mfululizo, kwa
yale makosa yasiyo na dhamana na yako ndani ya mamlaka ya Mahakama,
matumizi ya sheria yatumike ili kuyaondosha”, alisema.
Katika kupunguza msongamano magerezani, Jaji Mkuu amesema Maafisa wa
Mahakama hawana budi kutumia adhabu mbadala kwa makosa madogo madogo
kwa kuzingatia sheria zilizopo.