Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela (aliyevaa kofia nyeusi) akifanya mazoezi na wananchi wa Wilaya ya Songwe mapema leo kabla ya kuzindua Mkwajuni Jogging Club.
Wanafunzi na wanawake waliojitokeza wakiendelea na mazoezi mapema leo Wilayani Songwe kabla ya uzinduzi wa Mkwajuni Jogging Club.
Katibu wa CCM Mkoa wa Songwe Mercy Mollel (wa kwanza kushoto) akifanya mazoezi na wananchi wa Wilaya ya Songwe mapema leo kabla ya uzinduzi wa Mkwajuni Jogging Club.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe Eliniko Mkola (aliyevaa tracksuit ya bluu) akifanya mazoezi na wananchi wa Wilaya ya Songwe mapema leo kabla ya uzinduzi wa Mkwajuni Jogging Club.
******************
Wanafunzi wawili kutoka Wilayani Songwe wanatarajiwa kupewa nafasi ya Kupanda Mlima Kilimanjaro mwezi ujao ikiwa ni sehemu ya Kumbukumbu ya Miaka 20 ya Kifo cha baba Taifa hayati J. K. Nyerere itakayofanyika Oktoba 14 mwaka huu Mkoani Lindi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa ahadi hiyo mapema leo wakati wa mazoezi ya viungo na Uzinduzi wa Club ya Mkwajuni Jogging club ya Wilayani Songwe.
Kabla ya uzinduzi huo, Brig. Jen. Mwangela amewaongoza wananchi wa Wilaya ya Songwe kufanya mazoezi ya kukimbia yaani Jogging kwa takribani kilomita saba pamoja na kufanya mazoezi mbalimbali ya viungo.
Aidha amesema Mkoa wa Songwe tayari una jumla ya vijana 11 ambao wameshapanda Mlima Kilimajaro kama sehemu ya kuonyesha uzalendo wao na vijana hao ni wale ambao hupenda kufanya mazoezi.
“Wanafunzi fanyeni mazoezi kwa ajili ya afya ya mwili na akili pia tutachagua wanafunzi wawili ambao watapewa mazoezi na wana Kimondo Jogging Club, mazoezi hayo yanahusisha kupanda Mlima Rungwe angalau mara mbili ndipo muweze kupanda Mlima Kilimanjaro, nitajitahidi tupate wanafunzi wa kike na wa kiume mtuwakilishe”, Bri. Jen. Mwangela
Amesisitiza kuwa mazoezi ni mazuri kwa afya na ni ajira, pia amewapongeza wananchi wa Waliojitokeza kushiriki mazoezi hayo huku akiwasisitiza kuendeleza utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Kheri Kagya amesema kila mtu anapaswa kufanya mazoezi angalau kwa muda wa dakika 30 kila siku ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa husababisha vifo kwa zaidi ya asilimia 30.
Dkt Kagya amesema kufanya mazoezi huondoa mafuta yasiyotakiwa mwilini, husaidia mzunguko wa damu kufanya kazi vizuri na ukifanya mazoezi kwa muendelezo mwili utaweza kuepuka magonjwa ya mara kwa mara.
Bi Shuhudia Huseni Musa mkazi wa Mkwajuni Wilayani Songwe amesema amefurahia kufanya mazoezi licha kupata maumivu ya viungo kwakuwa ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanya mazoezi kama hayo.
Amesema kwa kufanya mazoezi kila siku kunaweza kusaidia kujikinga na magonjwa kama vile shinikizo la damu, kisukari, uzito uliozidi hivyo anawashauri watu wazima hususani wanawake wawe na tabia ya kufanya mazoezi.