NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
KATIBU wa itikadi ,siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole ,amewaasa viongozi wa kuteuliwa na kuchaguliwa kujiongeza kwa kuwa wabunifu ili kuacha alama ndani ya jamii.
Aidha amewataka wananchi kushirikiana katika masuala ya maendeleo ya jamii kwani maendeleo hayana chama .
Akizungumza katika hafla ya chakula cha hisani, kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa madarasa na madawati ,iliyoandaliwa na mkuu wa wilaya ya Kibaha,Polepole alisema baada ya kuteuliwa na mheshimiwa Rais ni lazima mhusika atengeneze uongozi uliotukuka kuwatumikia watanzania .
Anaeleza ,ugonjwa walionao baadhi ya viongozi wanashindwa kujiongeza kumpa heshima Rais dkt John Magufuli kutokana na uamuzi wa kuteuliwa.
Polepole,amempongeza mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ,kwa ubunifu wake ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na amemuahidi kumsemea mema.
“Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni ,mama nitakusemea ,hiki ulichokifanya ni kikubwa na viongozi wengine wanastahili kukiiga ,kwa maslahi ya watanzania ,ni lazima kiongozi aache alama katika jamii ,tengenezeni uongozi uliotukuka kwenye jamii zenu.”alifafanua Polepole.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo amesema licha ya mkuu wa wilaya kufanya maamuzi hayo ,lakini serikali ni sikivu na imeshafanya mambo makubwa katika sekta ya elimu ikiwemo elimu bure ambapo imeshatoa milioni bilioni 20.5 .
Pamoja na hilo, imeshatoa bilioni 7.2 kwa ajili ya kukarabati shule nne kongwe ikiwemo Kibaha.
Ndikilo aliwaomba wadau waendele kujitokeza kusaidia kuchangia sekta ya elimu ili kupunguza changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo,miundombinu ya madarasa ,nyumba za walimu na madawati.
Awali mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter alieleza tatizo la upungufu madarasa ilikuwa ni vyumba 65 ,lakini tangu kuanza kwa kampeni hii wameshapata fedha ambayo itaweza kujenga madarasa 40.
Amesema kwasasa imebakia madarasa 25 hivyo ameshukuru wadau kujitokeza kuwaunga mkono na ameomba ushirikiano huo uendelee.
Assumpter,ameomba jamii iondokane na dhana potovu kwamba ,ukianzisha ama kubuni suala la kuchangisha kwa ajili ya maendeleo kuna kuwa na rushwa ,au upigaji ,kwakuwa imani potovu kama hizo zinachelewesha maendeleo.