******************
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Ndugu Tabia Mwita amewataka Wananchi kuwa mstari wa mbele kujitolea katika miradi ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mh. Daktari John Pombe Magufuli.
Bi Mwita amezungumza hayo leo alipotembelea kukagua utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya.
Aidha ametoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kutoa kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 1.5 ambazo zimetumika katika ujenzi wa Hospitali hiyo ambapo maendeleo ya ujenzi yanafuraisha na kutoa Imani ya matumizi mazuri ya fedha hizo.
“Nimpongeze Mh. Rais Magufuli kwa moyo wa kutupambania wananchi ikiwa lengo ni kutuvusha katika changamoto tulizonazo, niwaombe wananchi wenzangu kuendelea kumtia moyo na kuunga mkono juhudi za maendeleo anazozifanya” alisema Mwita.
Pamoja na hayo Bi Mwita ameupongeza Uongozi wa CCM Wilaya ya Rorya kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi sambamba na Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ndio msimamizi wa mradi wa Hospitali Hiyo.