Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina na Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japani, Dkt. Shinichi Kitaoka wakipongezana mara baada ya kutia saini Marekebisho ya Makubaliano (Amendment of MoU) katika ushirikiano wao wa uwekezaji kwa pamoja barani Afrika. Wengine ni wadau mbalimbali kutoka Sekta za Umma na Binafsi waliohudhuria hafla hiyo.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina na Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japani, Dkt. Shinichi Kitaoka wakitia saini Marekebisho ya Makubaliano (Amendment of MoU) katika ushirikiano wao wa uwekezaji kwa pamoja barani Afrika. Wengine katika picha ni wadau mbalimbali kutoka Sekta za Umma na Binafsi waliohudhuria hafla hiyo
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, akiwa kwenye kikao na Kobe Nabuyuki kutoka Makao Makuu ya JICA ambaye ni msimamizi wa miradi ya Sekta ya Nishati nchini Tanzania. Katika Kikao hicho kilichofanyika Tokyo, Japani, walijadili kuhusu miradi mbalimbali ya Nishati nchini.
………………….
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japani (JICA) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wametia saini Marekebisho ya Makubaliano (Amendment of MoU) katika ushirikiano wao wa uwekezaji kwa pamoja barani Afrika.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina na Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japani, Dkt. Shinichi Kitaoka wametia saini Makubaliano hayo, Tarehe 30 Agosti 2019, katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) unaofanyika Tokyo, Japani na kushuhudiwa na Waziri wa Fedha wa Japani, Keisuke Suzuki pamoja na Wadau wa sekta ya Umma na binafsi.
Katika Makubaliano hayo, Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika zitaendelea kunufaika na uwekezaji wa pamoja wa JICA na AfDB unaofanywa katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Nishati.
Kwa upande wa Tanzania, hadi sasa JICA na AfDB, wakishirikiana na Washirika wengine wa Maendeleo wamehusika katika ufadhili wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 673 (Backbone) ya kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Tabora.
Vilevile, miradi mingine inayofadhiliwa kwa pamoja na JICA na AfDB ni pamoja na mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 514 kutoka Singida hadi Kenya kupitia Arusha na mradi wa upanuzi wa vituo vya kupoza umeme wa gridi vilivyopo Dodoma na Singida.
Aidha, katika Mkutano huo, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, alifanya kikao na Kobe Nabuyuki kutoka Makao Makuu ya JICA ambaye ni msimamizi wa miradi ya Sekta ya Nishati nchini Tanzania.
Katika kikao hicho, walijadili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa MW 300 kwa kutumia Gesi Asilia utakaojengwa mkoani Mtwara, mradi wa kuboresha miundombinu ya kusambaza umeme katika Jiji la Dodoma pamoja na mradi wa kuzalisha Umeme MW 200 kwa kutumia Joto Ardhi.
Mkutano wa TICAD 7 ambao unajadili Maendeleo ya Afrika katika Sekta mbalimbali, unatarajiwa kufikia kilele leo tarehe 30 Agosti 2019.