Choo kinachodaiwa kutotumika kutokana na kutokamilika
Vibanda vilivyofungwa baada ya biashara kuwa ngumu katika soko la Majengo Mapya
Sehemu ya katikati ya soko hilo imelimwa mboga baada ya kutokuwa na shughuli za biashara zinazoendelea
…………………….
Na Mwandishi wetu, Katavi
Kutokamilika kwa ujenzi wa choo cha soko la Majengo Mapya katika kata ya Kawajense katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kumelalamikiwa na wafanyabiashara wa soko hilo ambao walichangishwa shilingi 80,000 kila mmoja kwa ajili ya ujenzi wa choo cha soko hilo miaka minne iliyopita
Hali hiyo imepelekea wafanyabiashara wengine kuhama na hivyo kushindwa kuendelezwa kwa soko hilo
Wafanyabiashara hao wamedai kuwa kutokana na kutokuwa na wafanyabiashara wa kutosha katika soko hilo wamepata mdororo wa kibiashara
Bwana Mussa Mwanakulya ni mmoja wa wafanyabiashara wa soko la majengo mapya amesema mwezi oktoba mwaka 2017 walifanya mkutano na mbunge wa Mpanda mjini ambapo walitoa malalamiko yao
Aliongeza kuwa cha kushangaza diwani wa eneo hilo alipotakiwa kujibu aliwaambia kuwa soko hilo ni la CHADEMA
“Sisi tunamshangaa diwani kwanza tumempigia kura sisi halafu anatuambia kuwa tuko CHADEMA” alisema Mwanakulya
Naye Bi. Magreth Michael alisema waliwahi kuchangishwa fedha shilingi 15,000/- kwa hatua tatu ili wajengewe vibanda vya kuuzia mitumba lakini jambo hilo halikufanyika ambapo ameomba mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli kuingilia kati ili waweze kunusika
“Nina watoto nilikuwa nasomesha sekondari lakini kwa sasa wako nyumbani nimeshindwa kulipa ada” alisema Magreth
Akijibu malalamiko ya wafanyabiashara hao Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya bwana Grayson Mwalugala amekiri kuchangisha wafanyabiashara fedha kwa ajili ya ujenzi wa choo
Alifafanua kuwa walipata kiasi cha shilingi milioni tatu na kutafuta mzabuni wa kujenga choo hicho ambacho alisema kimekamilika kwa asilimia 95
Hata hivyo alidai kuwa mwaka juzi walinyang’anywa soko hilo na uongozi wa kata ambao walidai wataliendeleza soko hilo
Aidha amedai kuwa uongozi huo wa kata ulipokea kiasi cha shilingi 950,000/- kwa ajili ya kumalizia choo hicho lakini hajui fedha hizo walizifanyia nini
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambaye pia ni diwani wa kata ya Kawajense bwana Pius Buzumali alisema watajipanga kutenga bajeti ya maji kwa mwaka ujao wa fedha ili choo hicho kianze kutumika
Kuhusu mkakati wa kulifufua soko hilo bwana Buzumali alisema atakaa na wataalamu wa halmashauri kushauriana kuona waweke kitu gani ambacho kitafufua soko hilo kwani kwa sasa wafanyabiashara wengi wamekimbilia katika soko la kata ya jirani
“Labda tuweke dagaa, lakini sijui kama dagaa peke yake itatosha kufufua soko hilo ngoja tutaona wataalamu watakavyoshauri” alisema Buzumali