NA MWAMVUA MWINYI,RUFIJI
MENEJA wa kanda ya Mashariki wa kituo cha uwekezaji Tanzania TIC Venance Mashiba , ameeleza wanajikita katika uwekezaji wa viwanda ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali kuinua sekta ya viwanda na uwekezaji.
Akizungumza baada ya shughuli za kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kuchakata betri chakavu ( China Africa Business Council) Rufiji ,mkoani Pwani, alisema wameelekeza jitihada hizo hususan viwanda vinavyotokana na malighafi za kilimo na inayopatikana kwa ndani kwa wingi ambapo hutoa ajira na kuongeza pato la Taifa.
“Leo tupo hapa kushuhudia hafla hii, ambapo ni sehemu ya juhudi za kituo cha uwekezaji katika kuhakikisha kiwanda hiki kinapata mahitaji yake hadi sasa kinafunguliwa “alieleza Mashiba.
Aidha Mashiba alibainisha, huduma za uwekezaji ni mtambuka ambapo zinatolewa na taasisi mbalimbali ambazo taratibu zake zikigongana inasababisha baadhi ya changamoto ya ucheleweshaji wa huduma kwa wawekezaji.
Alisema ,kutokana na hilo kituo hicho , kiliimarisha huduma zake kwa kuongeza taasisi za serikali ambazo zinatoa huduma mbalimbali, vibali na leseni ili mwekezaji apate huduma mahala pamoja na sio kuzunguka .
Akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho,mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alimuelekeza mkuu wa wilaya ya Rufiji Juma Njwayo kusimamia mpango wa matumizi bora ya ardhi .
Aliwataka wakulima waheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji na wafugaji waheshimu wakulima huku akiyasihi makundi hayo kuacha kuvamia maeneo ya uwekezaji.
Ndikilo aliipongeza TIC kwa jitihada zake katika kukuza na kuvutia uwekezaji nchini na namna inavyohudumia wawekezaji na kusema katika mkoa huo hadi sasa vipo viwanda vitatu vinavyojishughulisha na uchakataji wa betri chakavu jambo ambalo linahitaji kujivunia.
Awali mkurugenzi wa kiwanda hicho ,Rashid Xian Ding alisema wametoa ajira kwa watu 100,wanasaidia shughuli za kijamii,kusomesha watoto,kusaidia huduma za afya kwa watoto na kutoa maji kwenye jamii inayowazunguka.