Eric Msuya,MAELEZO, Dsm
Pale ambapo mali ghafi kwa kiwanda cha kisasa inakuwa ni mabaki hatarishi, ni dhahiri hata jamii husika hufurahia kupata ahuweni hiyo kwa kuwa na thamani, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi. Evarist Ndikilo jana Wilayani Rufiji Mkoa Pwani alionesha furaha kuzindua kiwanda cha uzalishaji wa betri kinachotumia mabaki ya betri na kuzalisha betri za gari na pikipiki,
Mkuu huyo amepongeza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa utayari wake wa kuwa taasisi wezeshi na bunifu na kwamba wawekezaji wan je na hapa nchini huwezeshwa kwa haraka sana na hata kupewa mawazo ya miradi mizuri kulingana na mtaji wa muwekezaji.
Katika sherehe fupi ya uzinduzi iliyojumuisha makundi mbambali ya jamii ya Rufiji na viongozi wengine wa serikali, Mkuu wa Mkoa aliweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha kampuni ya Huatang – China cha kuchakata betri za magari na pikipiki zilizokwisha muda kasha huzalisha ‘lead engot’ ambayo hutumika kama malighafi kutengeneza betri mpya.
“Nawashukuru sana TIC kuwaongoza hawa ndugu zetu katika hatua zote za kuwekeza na hatimaye kufanikisha kuanzisha uwekezaji wao Wilayani (Rufiji Mkoani Pwani). Hii kwetu ni neema, na Rufiji inaenda kuwa juu” Alisema Mhe. Evarist Ndikilo.
Aidha Mkuu wa Mkoa amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Ding Xuan kwa kuthubutu kuanzisha kiwanda hicho Wilayani Rufiji, kwani wana imani kubwa kwa hatua hiyo na kwamba kiwanda hicho kitakuwa chachu ya kuvuta wawekezaji wengine, kuongeza ajira, kuleta maendeleo na fursa kwa wakazi wa Rufiji na Taifa kwa Ujumla.
Kwa upande mwingine, Bw. Ndikilo amewataka wananchi kuupokea mradi huo ambao pia ni mlinzi wa mazingira, na kuhimiza ushirikiano baina ya wao na mwekezaji ili kupitia mafanikio ya mradi wao akawe balozi mzuri wa kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wengine kwa wingi Mkoani Pwani.
Huatang ni miongoni mwa viwanda vichache katika Wilaya ya Rufiji ingawa kuna uwekezaji mwingi na mkubwa katika Mkoa wa Pwani ukilinganisha na Wilaya ya Kisarawe, Mkurunga na Pwani.
Hii ni kutokana na juhudi za Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli kuweka miundombinu wezeshi katika Wilaya hiyo ikiwamo umeme ambao unatarajiwa kuzalishwa kutoka Bwawa la Mto Rufiji kiasi cha Megawatts 2015, hatua ambayo itasaidia kuhamasisha na kuvutia uwekezaji zaidi ndani ya Wilaya ya Rufiji.
“Niwaombe Wananchi wa Nyamwage kushirikiana vizuri na Wawekezaji wetu wa kiwanda hiki. Ushirikiano ni Muhimu sababu hawa ndio mabalozi huko kwao kwamba sasa Rufiji inafaa kwa uwekezaji wa viwanda” Amesema Mhe. Evarist.
Katika sherehe hizo Meneja wa TIC, Kanda ya Mashariki Venance Mashiba, ameiwakilisha ameahidi kuendeelea kutoa ushirikiano kwa kiwanda, naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. Ding Xian amesema kwamba ameanzisha mradi huo ikiwa ni kuitikia wito wa Rais Dkt. Magufuli na Balozi wa China ambao wanawahamisha kuanzisha viwanda na wana matumaini kwamba mradi utakuwa na tija kwa wananchi katika kuleta ajira, soko la malighafi na pato kiujumla.