Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere mabadiliko ya Tabia ya Nchi, Prof.Pius Yanda akizungumza na Wanahabari katika mkutano uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo.
***************
NA EMMANUEL MBATILO
Watafiti na wanasayansi takribani 300 kutoka bara la Afrika na nje ya Afrika wanatarajia kushiriki Kongamano la kimataifa litakalojadili mjadala utakaojikita katika kuainisha jinsi matokeo ya tafiti yanaweza kusaidia katika jitihada za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kongamano hilo linatarajia kufanyika katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Oktoba 8 na 10 mwaka huu.
Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere mabadiliko ya Tabia ya Nchi, Prof.Pius Yanda amesema kuwa kongamano hilo litatoa nafasi kwa wanasayansi kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali katika maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
Aidha Prof.Yanda amesema kuwa wanawaalika watafiti,wana taaluma na wale wote wanaoshiriki katika shughuli za kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi kwa njia moja au nyingine pamoja na wale wote watakaoopenda kushiriki.
“Kongamano hilo litajikita katika maeneo ya Usimamizi wa maliasili na mifumo yake ya ki-ekologia katika kipindi chenye changamoto ya mabadiloko ya Tabia Nchi, Mabadiliko ya Tabia nchi na Usalama wa Chakula pamoja na nyingine ya Ubunifu wa Teknolojia, maadili katika usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya Tabia Nchi”. Amesema Prof.Yanda.