……………………………..
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeupongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa na barabara ya kuunganisha mkoa kwa mkoa kupitia mtandao wa barabara nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji ya Wakala huo ilyowasilishwa kwa Wajumbe wa Kamati jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso, amesema kuwa kupitia utaratibu huo hata barabara zilizosahaulika nchini zinaweza kunufaika kwa kuwa na maendeleo ya kiuchumi kutokana na uwepo wa miradi hiyo.
“Naipongeza Serikali kupitia TANROADS kwa kufikiria kuunganisha mikoa kupitia barabara hususan katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mikoa hii ilionekana kama imesahaulika lakini sasa inaonekana kupata maendeleo kutokana na uwepo wa miradi ya barabara ambayo inatekelezwa”, amesema Mhe. Kakoso.
Aidha, Ameutaka Wakala huo kuendelea kuziangalia na kuzipa kipaumbele barabara za kimkakati ambazo zina maslahi mapana katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ametaja miradi hiyo kama barabara ya Mtwara- Mnivata, Katavi- Kigoma na Kasulu – Kagera ambayo kwa pamoja ikikamilika itaunganisha mikoa hiyo na mikoa jirani na hatimaye kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Mwenyekiti Kakoso, ameusisitiza Wakala huo kuendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege hususan katika ujenzi wa majengo ya abiria ambayo yanaendana na wingi wa abiria pamoja na kujenga uzio katika viwanja vya ndege ambavyo havina uzio lengo likiwa ni kuweka usalama katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na mizani.
Amefafanua kuwa hadi kufikia Juni, 2019 Wakala umefanikiwa kujenga kituo cha mizani cha Kurasini ambacho kimejengwa kwa ajili ya kuhakiki uzito wa magari yanayotoka bandarini na kuweka CCTV Kamera katika mzani huo.
Kwandikwa, ameongeza kuwa Wakala umeendelea na kazi za ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege ambapo hatua za utekelezaji zilizofikiwa kwa baadhi ya miradi zinaridhisha.
Amesema kuwa hadi kufikia Juni, 2019 ujenzi wa Jengo la abiria katika Kiwanja cha ndege wa Songwe umefika asilimia 77 na ukarabati na ujenzi wa Jengo la kuongozea ndege na mizigo katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza umefika asilimia 93.
“Sisi kama Serikali tutaendelea kuboresha viwanja vingine vya ndege, tunajua wananchi wanahitaji maendeleo kupitia sekta ya anga, hivyo hatuna budi kuboresha viwanja hivi, amesisitiza Kwandikwa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepokea taarifa ya TANROADS ambayo imeainisha majukumu ya Wakala huo kwa mwaka wa Fedha 2018/19 na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara kuu, barabara za mikoa, madaraja na viwanja vya ndege.