TIMU ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) imetupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa 2-1 na AS Kigali ya Rwanda jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
KMC iliyotoa sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza mjini Kigali inaicha AS Kigali isonge Raundi ya michuano hiyo ambako itamenyana na mshindi kati ya Proline ya Uganda na Masters Security ya Malawi. Proline ilishinda 3-0 mechi ya kwanza nyumbani na timu hizo zinarudiana kesho Malawi.
Katika mchezo wa leo, AS Kigali ilitangulia kwa bao Rashid Kalisa dakika ya 29 akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya KMC inayofundishwa na kocha Mganda, Jackson Mayanja.
KMC ilijaribu kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa AS Kigali kusaka bao la kusawazisha, lakini vijana wa kocha Eric Nshimiyimana walifanikiwa kuzuia hatari zote.
Kipindi cha pili, nyota ya timu ya Kigali iliendelea kung’ara baada ya kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 70 kupitia kwa Eric Nsabimana aliyemalizia pasi ya Janvier Benedata kufunga kwa urahisi baada ya kipa Juma Kaseja kutoka langoni kujaribu kuwahi kuokoa.
KMC ilifanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 88 kupitia kwa kiungo Mrundi, Yusuph Ndikumana aliyefunga kwa penalti iliyotolewa na refa Sabri Mohammed Fadul kutoka Sudan baada ya mchezaji wa AS Kigali kuunawa mpira kwenye boksi.
Kikosi cha KMC kilikuwa; Juma Kaseja, Amos Kadikilo, Abdallah Mfuko, James Msuva/ Vitalisy Mayanga dk46, Yussuf Ndikumana, Hassan Kabunda, Boniphace Maganga, Ally Msengi, Abdul Hilaly/Mohammed Samata dk47, Kenny Ally na Salim Aiyee.
As Kigali: Shamiru Batte, Latif Bishira, Christian Ishimwe, Farouq Ssentengo, Janvier Benedata/Nova Bayama dk80, Tumaini Ntamuhanga, Rashid Kalisa, Ibrahim Nshimiyimana, Michael Rusheshangoga, Shaffi Songayingabo na Eric Nsabimana.