Home Mchanganyiko WAWEKEZAJI BINAFSI WA UMEME NCHINI WANACHANGIA ASILIMIA 13 KATIKA GRIDI – MGALU

WAWEKEZAJI BINAFSI WA UMEME NCHINI WANACHANGIA ASILIMIA 13 KATIKA GRIDI – MGALU

0

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akiongoza kikao cha majumuisho kilichohusisha wataalamu wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kushiriki kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma, Agosti 23, 2019.

………………………………………………….

Na Veronica Simba – Dodoma

Serikali imeendelea kutoa fursa kwa wawekezaji binafsi katika kuzalisha umeme nchini ambapo hadi sasa wanachangia asilimia 13.5 katika gridi ya taifa.

Hayo yameelezwa leo, Agosti 23, 2019 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Aidha, amesema kuwa serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), imetangaza zabuni kwa ajili ya wawekezaji binafsi kuwekeza katika miradi mipya ya kufua umeme, ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 950.

Akifafanua, amesema mchanganuo wa megawati hizo unahusisha umeme jua (megawati 150), upepo (megawati 200) na makaa ya mawe (megawati 600).

Akizungumzia utoaji fursa kwa wawekezaji wadogo wenye nia ya kuzalisha umeme nchini, Mgalu amesema, ili kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wawekezaji hao, serikali tayari imeandaa sheria na bei elekezi ambazo zilichapishwa katika gazeti la serikali Juni 21, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka ameiambia Kamati hiyo ya Bunge kuwa hali ya upatikanaji umeme nchini ni nzuri ukilinganisha mahitaji yaliyopo kwa sasa na uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme.

Kuhusu hali ya uzalishaji umeme nchini, Dkt Mwinuka amesema hadi kufikia Agosti 6 mwaka huu, uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa gridi ya taifa ulifikia megawati 1, 565.72

Aidha, amesema, shirika linamiliki mitambo ambayo haijaunganishwa katika mfumo wa gridi ya taifa yenye uwezo wa kuzalisha takribani megawati 36.176 hivyo kufanya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kufikia jumla ya megawati 1,601.896

Ameongeza kuwa, mahitaji ya juu ya umeme katika gridi ya taifa yalifikia megawati 1,116.58 Novemba 30 mwaka jana ikilinganishwa na megawati 1,051.27 zilizokuwa zimefikiwa hadi Juni, 2018.

“Kwa mlinganisho wa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme na mahitaji yaliyopo, kuna ziada ya wastani wa megawati 300 katika gridi ya taifa. Taifa litaendelea kuwa na umeme wa ziada kutokana na miradi ya ufuaji umeme inayotekelezwa,” amefafanua.

Kikao hicho cha Kamati ya Bunge kimehudhuriwa pia na viongozi na wataalamu mbalimbali wa Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini yake.