Home Michezo Mchezo wa Riadha Watia fora Mashindano ya FEASSSA Jijini Arusha

Mchezo wa Riadha Watia fora Mashindano ya FEASSSA Jijini Arusha

0

Baadhi ya wanariadha wa Tanzania walioshinda medali za dhahabu, fedha na shaba wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mashindano ya riadha ya FEASSSA yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo.

Kocha wa timu ya taifa ya riadha na mshauri wa ufundi wa timu ya riadha ya Tanzania kwenye michuano ya FEASSSA Robert Kalyahe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washindi wa riadha kutoka Tanzania leo.

Washindi wa kwanza wa mchezo wa mbio za kupokezana kijiti mita 100 x 4  kutoka Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mbio zao leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha

…………………

Na Mathew Kwembe, Arusha

Mashindano ya michezo ya shule za Sekondari kwa nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA) imeingia katika siku ya nane leo ambapo mbali na michezo mingine inayoendelea kulifanyika pia mchezo wa riadha ambapo wanariadha kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania walitia fora baada ya kujizolea pointi na medali nyingi katika michuano hiyo.

Hadi michezo hiyo inakamilika leo mchana, timu ya wanariadha kutoka nchini Kenya ndiyo inayoongoza kwenye mashindano hayo kwa upande wa riadha kwa kujishindia jumla ya pointi 345 kufuatia wanariadha wake kupata medali 18 za dhahabu, 9 za fedha na 10 za shaba na jumla kujizoelea medali 37.

Nafasi ya pili katika mchezo wa riadha ilichukuliwa na wanariadha kutoka Uganda ambao walijizolea pointi 316 baada ya kushinda medali 8 za dhahabu, 14 za fedha na 10 za shaba huku wenyeji Tanzania wakiambulia nafasi ya tatu baada ya kupata jumla ya pointi 197 kwa kupata medali 2 za dhahabu, 5 za fedha na 6 za shaba.

Mchanganuo wa matokeo hayo unaonyesha kuwa  ushindi wa Kenya umechangiwa na wanariadha wake wasichana kwa wavulana kufanya vizuri katika mashindano hayo ambapo timu yake ya wasichana ilijizolea medali 7 za dhahabu, 4 za fedha, na 6 za shaba na hivyo kujinyakulia pointi 162, huku wanariadha wavulana kutoka nchi hiyo walifanikiwa kupata medali 11 za dhahabu, 5 za fedha na 4 za shaba,

Kwa upande wa Uganda ushindi wao ulitokana na mafanikio ya wanariadha wao wasichana ambao walipata medali 5 za dhahabu, 8 za fedha na 4 za shaba na kujizolea jumla ya pointi 165, huku wavulana walipata medali 3 za dhahabu, 6 za fedha na 3 za shaba

Tanzania kwa upande wao timu yao ilishika nafasi ya tatu kufuatia timu yao ya wasichana kujishindia medali 2 za dhahabu, 2 za fedha na 4 za shaba na jumla kupata pointi 104 huku wavulana kutoka Tanzania walipata medali 3 za fedha na 2 za shaba.

Waliofanikiwa kuiletea medali ya dhahabu Tanzania ni mwanariadha Carreen Philipo kutoka shule ya sekondari ya wasichana Kondoa iliyopo mkoani Dodoma, mwanafunzi wa kidato cha tano ambaye alifanikiwa kushinda medali hiyo baada ya kufanikiwa kurusha tufe umbali wa mita 12.71 na kuwashinda Penina Akoth wa Kenya na Alanyo Catherine wa Uganda ambao walishika nafasi ya pili na tatu.

Medali nyingine ya dhahabu ilitokana na ushindi wa timu ya wasichana ya Tanzania katika mchezo wa kupokezana vijiti mita 100 x 4 ambapo wasichana wanne kutoka Tanzania walifanikiwa kushika nafasi ya kwanza mbele ya wanariadha wa Kenya na Uganda.

Akizungumzia michuano hiyo Kocha wa riadha wa Tanzania Taratibu Machaku amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yalikuwa magumu kuliko walivyodhani lakini amewasifu vijana wake kwa ushujaa waliouonyesha kwenye mashindano hayo licha ya ukweli kuwa wanariadha wengi wa Tanzania hawatoki kwenye shule za michezo kulinganisha na wanariadha kutoka Kenya na Uganda.

Hivyo Machaku amewataka wadau wa michezo nchini kujenga shule nyingi za kulea vipaji vya michezo nchini ili Tanzania iweze kuwa na timu imara ya kuweza kushindana na nchi za Kenya na Uganda.

Naye Mwanariadha  Mathayo Sombi wa Tanzania, Mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka shule ya vipaji ya Alliance ya jijini Mwanza ambaye alifanikiwa kupata medali 2 za fedha baada ya kushika nafasi ya pili katika mbio ndefu za mita 10,000 na mita 5,000 alisema kuwa hali ya hewa ya Arusha ilichangia kumuathiri kushinda nafasi ya kwanza na amesema anajipanga mwakani ili aweze kushinda mashindano hayo.

Kwa upande wake Felix Ogwang ambaye ni mwandishi wa michezo kutoka Uganda amesema kwa upande wake ameona vipaji vingi vya michezo kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania lakini kwa maoni yake ameona kuwa kinachowakosesha ushindi wanariadha wa Tanzania ni kuchukulia michezo kama kitu cha ziada cha kufanya baada ya masomo.

Amesema kuwa hali hiyo ni tofauti na Uganda kwani wanafunzi wanaoshiriki michuano mikubwa ya FEASSSA ambao hupewa cheti maalum na wizara ya elimu ya Uganda hupata alama 5 ambazo hujumlishwa kwenye matokeo ya kujiunga na elimu ya juu nchini humo jambo ambalo Ogwang ameliita kama motisha inayowavuta vijana wengi nchini humo kujituma zaidi katika michezo.

Mashindano ya 39 ya FEASSSA yanatarajiwa kukamilika tarehe 25 agosti 2019 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo jumla ya mataifa sita ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi na wenyeji Tanzania yalishiriki mashindano hayo.