*******************
Na. Catherine Sungura, Dodoma
Wauguzi wote nchini wametakiwa kufanya kazi kwa pamoja na kuacha tabia za
ubinafsi ili kuweza kuwasaidia wananchi wanaofika kwenye vituo vya kutolea
huduma za afya kupata huduma bora na kwa wakati.
Hayo yamesemwa na katibu mkuu Wizara ya afya Dkt. Zainab Chaula
aliposhiriki kikao cha kuwashirikisha wadau mwongozo wa utoaji huduma kwa
kuzingatia utu,heshima na maadili kilichofanyika jijini hapa.
Dkt. Chaula alisema kuwa taaluma ya uuguzi ni ya wito hivyo wanatakiwa
kuzingatia weledi wa fani yao ili kuwa na mafanikio ya utoaji huduma za afya
nchini ili kuokoa maisha ya watanzania ambao wanahitaji msaada wa kuokoa
kutoka kwa wataalam hao.
“Lazima turudishane kwenye mstari ili tuweze kuokoa maisha ya akina mama
wajawazito,watoto na wagonjwa wengine ,tujiulize kwanini akina mama
wajawazito wanafariki?nyinyi ndio chachu ya mabadiliko katika utoaji wa
huduma”.Alisisitiza Dkt.Chaula.
Aidha, katibu mkuu huyo alisema kuwa katika kutimiza wajibu wa wauguzi
kwenye vituo vya kutolea huduma za afya anatamani kusiwepo na kifo hata
kimoja hususani upande wa akina mama wajawazito hivyo inahitajika nguvu ya
pamoja na uelewa miongozi mwa wauguzi kote nchini ili ifikapo 2020.
Mkakati wa kitaifa wa kupunguza vifo wa vitokanavyo na uzazi tanzania
imekusudia ifikapo mwaka 2020 kupunguza vifo hivyo kufikia 292 katika vizazi
hai laki moja ukilinganisha na mwaka 2015 vya vifo 556 kwa vizazi hai laki
moja.