………………………………….
NA.MWANDISHI WETU
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inayojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi na Ukimwi imeendesha warsha kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI kuwaeleza kuhusu shughuli wanazotekeleza pamoja na kujadiliana namna ya kushirikiana kufikisha huduma za VVU na Ukimwi kwa wananchi.
Warsha hiyo imefanyika Agosti 21, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Utawala bungeni Dodoma na kukutanisha pamoja wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya sheria ndogo pamoja na maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na TACAIDS.
Awali akizungumza katika warsha hiyo,Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt, Leonard Maboko alisema wameona ni vyema kukutana na wajumbe wa kamati hizo ili kuwaeleza shughuli zinazofanywa na Tume pamoja kutoa elimu kuhusu masuala ya Ukimwi nchini.
“Tumefanya semina hii kwa lengo la kuwapitisha wabunge juu ya majukumu ya Tume kisheria na kueleza mikakati, miongozo ya Kitaifa iliyopo na itayosaidia wadau mbalimbali katika kuratibu masuala mbalimbali ya Ukimwi hapa nchini,”alieleza Dkt. Maboko
Aliongezea kuwa, kukutana na wajumbe wa kamati hizo kumewapa fursa ya kutoa elimu na kupokea mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe hao ili kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Tume hiyo.
Aidha alifafanua kuwa kwa kuzingatia masuala ya VVU na Ukimwi ni mtambuka, hivyo ni vyema kuendelea kutoa elimu kuhusu masuala hayo na kuhakikisha wanaendelea kuboresha na kuisaidia jamii katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
“Lazima tuhakikishe tunaendelea kutekeleza zile 909090 kwa kuangalia utekelezaji wake kwani malengo ya kidunia yanaeleza kuwa, ifikapo mwaka 2020 tunatarajia kuona watanzania wanaoishi na Virusi vya Ukimwi asilimia 90 wawe wameshajua hali zao za maambukizi, na ile tisini ya pili wawe wameshaanza kutumia dawa na 90 ya mwisho wawewameanza kufubaza virusi vya Ukimwi ambapo hadi sasa ni asilimia 87 ya Watanzania wanatumia dawa,”alieleza Dkt.Maboko.
Alifafanua kuwa malengo na majukumu ya Tume ni kuona ifikapo mwaka 2030 kusiwe na maambukizi mapya kwa kuzingatia sifuri tatu ambazo zinaeleza kutokuwa na vifo vinavyotokana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (vifo sifuri) na kusiwe na unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo,Mheshimiwa Oscar Mukasa alipongeza Tume kwa jitihada inazozifanya katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi huku wakiomba waendelee kuelimisha umma hususan maeneo yasiyofikika kiurahisi ikiwemo vijijini kwa kuzingatia athari zitokanazo na Janga hilo.
Aidha alishauri Serikali kuendelea kuwafikia wanaoishi vijijini kwa kuwapa vipaumbele na kutumia mbinu rahisi za kufikisha elimu ikiwemo matumizi ya sanaa na michezo inayowazunguka katika mazingira yao.
“Wito wangu Tume, mngeangalia namna bora ya kuwafikiwa walioko vijijini katika kuwapatia elimu kwa kuzitumia tamaduni zetu mfano kupitia ngoma za asili na michezo ikiwa ni moja ya mkakati katika kufikisha ujumbe,”alisema Mukasa
Naye mjumbe wa kamati kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Mheshimiwa William Ngeleja alieleza kuwa, wamefarijika kwa semina hiyo na kuendelea kutoa wito kwa Serikali kuendelelea kuongeza jitihada katika kuwafikia walengwa wengi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa katika kuunga jitihada zinazofanywa na Tume hiyo.
“Niiombe jamii kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini kwa kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa balozi katika vita hii hatimaye tuwe na taifa imara lenye wananchi wenye afya ili washiriki katika shughuli za kimaendeleo,”alisisitiza Mhe. Ngeleja.