Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais akimkaribisha Mgeni Rasmi katika Warsha ya Maafisa Mazingira wa mikoa ya Tanzania Bara ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine(aliyekaa) ili aweze kuzungumza na Maafisa hao. Warsha hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanyika jijini Dodoma.
************
Maafisa Mazingira Nchini wametakiwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais ili kuhakikisha Katazo la mifuko ya plastiki linafanikiwa na kutekelezeka vema.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine alipokutana na Maafisa hao kutoka mikoa ya Tanzania Bara katika Warsha iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika ukumbi wa Nyaraka jijini Dodoma.
Alisema kuwa Warsha hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ina lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wakatazo la mifuko ya plastiki na namna ya kuboresha ushirikiano na uratibu katika hifadhi ya mazingira kwa ujumla.
“Kwa ujumla, katazo la mifuko ya plastiki limeleta sifa na heshima kwa nchi yetu katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa. Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi 60 duniani ambazo zimepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. Hii ni hatua kubwa na ya kujipongeza kwa dhamira na msimamo wa Serikali katika
kukabiliana na changamoto za hifadhi ya mazingira” alisema Balozi Sokoine.
Aliongeza kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni kuibuka kwa matumizi ya mifuko ya plastiki ya kubebea bidhaa ambayo ni “transparent” na kupelekea mifuko hiyo kuzagaa na kutumiwa kama vibebeo vya kubebea bidhaa. Hivyo basi amewaagiza Maafisa hao wa Mikoa kuanza kufanya ukaguzi kwa kushirikiana na Baraza la Usimamizi wa Mazingira katika mikoa yao waliotoka.
Pia aliwasisitiza kuendelea kujenga uelewa kwa walio chini yao kuanzia ngazi ya
mkoa mpaka ngazi ya chini(kata,Tarafa,vijiji) ili elimu ya katazo la matumizi ya mifuko ya plstiki ifike mpaka ngazi ya chini.
Katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki lilianza rasmi tarehe mosi ya mwezi juni 2019, ikiwa ni kufuatia agizo lilitolewa na Mh. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bungeni jijini Dodoma.
Ofisi ya Makamu wa Rais ni wasimamizi wakubwa katika kampeni hiyo ya marufuku ya mifuko ya plastiki.