Zaidi ya waumini elfu 35 wa kanisa la kiinjili la kilutheli Tanzania KKKT jimbo la Mufindi lililopo mkoani Iringa wameanza mchakato wa kujitenga kutoka dayosisi ya kusini kwa madai ya kwamba wamechoshwa na vitendo vya ukikwaji wa katiba unaofanywa na viongozi wa dayosisi hiyo akiwemo askofu mkuu wa dayosisi ya kusini Isaya Mengele.
Ikifafanua sababu ya kujiondoa katika dayosisi hiyo ,kamati ya maandalizi ya uanzishwaji wa dayosisi ya Mufindi kusini akiwemo Odenburg Mdegela askofu mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa na Maltin Ngwembe ambaye ni mwenyekiti wa mchakato huo wa kujitenga wanasema wamelazimika kushinikiza kujietenga kwasababu ya uongozi mbovu,Ulaghai,Vitisho pamoja na kutofikiwa na huduma kutokana na ukubwa wa dayosisi hiyo.
Wawakilishi hao wa waumini wa Jimbo la Mufindi wamesema wamekuwa wakidai haki ya kujitenga tangu 1984 bila mafanikio kwasababu dayosisi inaongozwa na viongozi ambao wamekuwa wakinufaika na ukubwa wa mazingira ya utawala jambo ambalo linawafanya kutengeneza kila aina ya hujuma ili Jimbo la Mufindi lisimeguke kutoka dayosisi ya kusini.
Kwa mujibu wa katiba ya KKKT ili dayosisi iweze kuundwa inapaswa kuwa na waumini wasiopungua elfu 10 jambo ambalo linalifanya jimbo la Mufindi kukidhi sifa kwa kuwa inawaumini zaidi ya elfu 35 na kwamba zuio la kujitenga kwao linatokana na utajiri mkubwa wa jimbo la mufindi na kiwango cha mchango wake kwenye dayosisi na kanisa kwa ujumla.
Kwa upande wao wajumbe wa kamati ya kumeguka kutoka dayosisi ya kusini yenye makao makuu mjini Njombe akiwemo Mariam Mtisi na Yohana Kilunga wamechoshwa na mwenendo wa dayosisi hiyo kwa kuwa imekuwa ikiwakandamiza wachama pamoja na vitisho na kwamba wakati umefika wakuondoka changamoto ya kuongozwa na Askofu Isaya Mengele ambaye wamemtuhumu kwa kukiuka katiba ya KKKT.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa waumini wa wilaya ya Mufindi lakini huko Njombe miezi kadhaa iliyopita kiliibuka kikundi cha watu wanne ambao walikuwa wakimpinga askofu Isaya Mengele na uongozi wake.
Tayari waumini wa KKKT jimbo la Mufindi wameanza ujenzi wa kanisa kubwa lenye hadhi ya dayosisi litakalo gharimu zaidi ya bil 2.