Baadhi ya maafisa elimu maalum na elimu ya watu wazima akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati mara baada ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao,leo katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akiteta jambo na Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga wakati wa kufungua kikao kazi cha maafisa elimu Mkoa, Maafisa elimu maalum na maafisa elimu ya watu wazima,leo katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
Baadhi ya maafisa elimu maalum na elimu ya watu wazima akiwa katika wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ( hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi cha maafisa hao,leo katika ukumbi wa mikutano
wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
**************
Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
Nchini kuhakikisha wanawezesha maafisa elimu nchini kwa kutenga bajeti
kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Elimu Mikoa,
Maafisa elimu maalum na maafisa elimu ya watu wazima kilichofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha mipango, Jijini Dodoma.
Amesema kuwa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri hawatoi
kipaombele katika masuala yanayohusu elimu maalum na elimu ya watu
wazima katika Halmashauri zao jambo ambalo linafanya maafisa wa idara
hizo kuwa wanyonge na kukata tamaa ya kutekeleza majukumu yao kwa
wakati.
“Maafisa elimu wanaosimamia elimu maalum na elimu ya watu wazima
wako choka mbaya katika Halmashauri nyingi nchini, hata ukihesabu na
kutaka viongozi wa Halmashauri wengi hawasimami kwa sababu ya
kutojiamini na kujiona wametengwa na jamii hii inaleta sura mbaya na
kusababisha watu walioko kwenye kundi hili kusahaulika na kutotimiziwa
mahitaji yao kwa wakati” Amesema Jafo.
Mhe. Jafo anafafanua kuwa maafisa elimu maalum na elimu ya watu
wazima hushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kutotengewa fedha na
kuonekana si vipaombele vya Halmashauri, jambo ambalo linasababisha
watoto wengi wenye mahitaji maalum na watu wazima kushindwa kupata
elimu bora sawa na watu wengine.
“ Afisa elimu maalum akiwa na kazi maalum lazima aombe msaada wa gari
kutoka Idara nyingine,hivyo nawaagiza wakurugenzi kuhakikisha katika
bajeti zenu za ndani kutenga fedha kwa ajili ya maafisa elimu maalum na
elimu ya watu wazima ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo”
Amesisitiza Mhe. Jafo.
Mhe. Jafo amewataka kuhakikisha wanaainisha vipaombele vya elimu
maalum na watu wazima na kuviingiza katika bajeti ya Halmashauri husika ili kuziwezesha Idara hizo kupanga mipango yao na kuitekeleza kwa wakati.
Wakati huohuo, amemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa kuhakikisha kila Halmashauri inaainisha kwenye bajeti
zao vipaombele vya Elimu Maalum na Elimu ya watu wazima katika
mchakato mzima wa bajeti na kuwekewa fungu katika Halmashauri zote
nchini.
Amemtaka kuhakikisha anafanya uhakiki kwa kila mkoa pindi inapoleta
bajeti yake kama wameweka vipaombele vya elimu maalum na elimu ya
watu wazima, kama ilivyofanywa kwa asilimia kumi ya kuwawezesha
vijana, wanawake na walemavu ili kuyafikia makundi hayo.
Mhe. Jafo amesema bila kufikia mahali na kuona ni kipaombele cha
Halmashauri kuhakikisha kundi la watu maalum na elimu ya watu wazima
linahudumiwa katika jamii, kundi hili litakuwa likitegemea wafadhili pekee
jambo ambalo si malengo ya Serikali.
Vilevile amewaagiza maafisa elimu Maalum na watu wazima kuhakikisha
wanatembelea maeneo yao ya kazi ili kutatua matatizo ya kundi hili katika
maeneo wanayofanyia kazi.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema kuwa malengo ya mkutano huu ni
kuwapa uelewa Maafisa elimu kuhusu mpango mkakati wa elimu jumuishi
kuwa ni ajenda muhimu katika maeneo yao ya kazi, kuwajengea uwezo wa
namna ya kukuza na kusimamia maadili ya uongozi wa utumishi wa umma
na dhana nzima ya ugatuaji wa madaraka na kuendesha na kusimamia
programme mbalimbali za maendeleo ya elimu nchini.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa anayeshughulikia elimu Tixon Nzunda amewaomba wadau wa elimu
nchini kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake katika kutatua
changamoto mbalimbali za elimu nchini kwa kufuata vipaombele
vinavyotolewa na kinyume chake watapingana na juhudi za Serikali.