Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile (katikati) akizungumza na vyombo vya habari leo Jijini Dodoma kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia, kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Jinsia Bi. Mboni Mgaza na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Jinsia Bw. John Mapunda.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
………………………
Na Anthony Ishengoma WAMJW
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa mtoto wa kike uzidi kukua kiuchumi kulingana na muda anaokaa shuleni akiongeza kuwa mwanamke anavyozidi kujiendeleza kielimu upunguza uwezekano wa kuwa na idadi kubwa ya watoto na na kufanyiwa vitendo vya kikatili.
Dkt. Ndugulile amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa akiitambulisha Kampeni mpya ya Kitaifa ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ijulikanayo kama Twende Pamoja inayolenga kushirikisha wanaume na wanawake kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kupitia mbinu anwai.
Aidha Dkt. Ndugulile amesisitiza kuwa kuwepo kwa elimu bure nchini kwa kiasi kikubwa kumepunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo mimba na ndoa za utotoni pamoja na uwepo wa Sheria inayotoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa anayebainika kufanya vitendo hivyo.
Dkt. Ndugulile ametaja wastani wa watoto kwa mwanamke wa Tanzania kuwa watano hivyo kadri msichana anavyokaa shuleni anapunguza uwezekano wa wa kuzaa watoto wengi lakini pia akasema uwezi ukalinganisha kipato cha Msichana wa kidato cha nne na yule wa Darasa la Saba.
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya kampeni hiyo Dkt. Ndugulile ameviambia vyombo vya habari kuwa yeye kama Naibu Waziri anachukizwa na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake hivyo akachukua fursa hiyo kuhamasisha pia wanaume wengine nchini kuchukia vitendo hivyo akiitaja kauli mbiu ya Kampeni hiyo kuwa ni ”Ukatili wa Kijinsia Tanzania sasa basi’’.
Akizungumzia hali ya ukatili wa kijinsia Nchini Dkt. Ndugulile amesema taarifa ya hali ya Uhalifu nchini ya Mwaka 2017 inaonesha kuwa jumla ya watu 41,416 waliofanyiwa ukatili wa kijinsia walitoa taarifa kwenye vituo vya polisi ikilinganishwa na watu 31,996 waliofanya hivyo mwaka 2016.
Dkt. Ndugulile ameyataja baadhi ya matukio ya ukatili yaliyotolewa taarifa kuwa ni ubakaji, vipigo, matusi, ulawiti, kutupa watoto, ukeketaji na kuwapa mimba wanafunzi na kuongeza kuwa kati ya mataukio hayo 41,416 yaliyotolewa taarifa mwaka 2017 matukio 27,703 sawa na asilimia 67 yalifanywa dhidi ya wanawake na watoto.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa asilimia 40 ya wanawake wa umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi hicho cha maisha wakati wanawake asilimia 20 wenye umri miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Dkt. Ndugulile amefafanua kuwa Wizara ianshirikiana na wasanii katika kufikisha ujumbe na amemtaja Msanii Nurdin Bilal Maarufu SHETTA kuwa amejitolea kuwa Balozi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto na atataumia jukwaa la Sanaa kuelimisha jamii kwa kutumia mziki wake na mitandao ya kijamii.
”Ni matarajio yangu kwamba kampeni hii ya Kupinga Ukatilili wa Kijinsia Kitaifa italeta mabadiliko makubwa kupitia jumbe mbalimbali zilizoandaliwa kupitia muziki, machapisho, nyimbo, shuhuda na Semina zitakazokuwa zinaendelea kutolewa kwenye majukwaa mbalimbali kipindi cha kampeni’’. Alihitimisha Dkt. Ndugulile.