KAMPUNI ya Michezo ya Kubahatisha ya M-bet imeingia mkataba wa miaka mitano kuidhamini klabu ya KMC wenye thamani ya Sh. Bilioni 1.
Mkataba huo umesainiwa leo mjini Dar es Salaam katika shughuli iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa jezi za msimu mpya za timu hiyo inayomilikiwa na Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Habari hizo njema zinakuja KMC siku mbili kabla ya kuteremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na AS Kigali katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza kombe la Shirikisho Afrika.
KMC watakuwa wenyeji wa AS Kigali, timu mpya ya kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Haruna Niyonzima keshokutwa katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho, wakihitaji ushindi wowote kusonga mbele baada ya sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza Rwanda.
KMC iliyopanda Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, moja kwa moja imetokea kuwa moja ya timu tishio nchini na msimu imepata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo, nyuma ya Azam FC.
Bingwa na mshindi wa pili wanacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati mshindi wa tatu anaungana na mshindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kucheza Kombe la Shirikisho.
Na kwa kuwa Azam FC ndiye mshindi wa Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), KMC imepata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na kumaliza nafasi ya nne.