Na.Alex Sonna,Ikungi
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe Edward Mpogolo amepongezwa kwa namna ambavyo ameweza kusimamia miradi ya maendeleo ndani ya muda mfupi tangu ateuliwe kwenye nafasi hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ally wakati Mwenge wa Uhuru ulivyofika kukagua miradi ya maendeleo wilayani Ikungi.
Miradi mitano ya Maendeleo iliyokaguliwa na kuzinduliwa ni pamoja na vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Darajani, Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Ighuka, Mnara wa Mwenge wa Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere na Ukumbi wa Halmashauri ya Ikungi ambapo miradi yote hiyo imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.162.
Akizungumza Wilayani hapo Kiongozi huyo amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kufanya kazi kwa uzalendo ili kuwafanya Watanzania waendelee kuiamini Serikali yao chini ya Rais Dk John Magufuli.
” Niwapongeze sana Wananchi wa Ikungi kwa namna ambavyo mmeendelea kumuamini Rais wetu Dk Magufuli, kipekee nikupongeze DC Mpogolo kwa uzalendo wako unaouonesha toka uteuliwe na Mhe Rais kuwa Mkuu wa Wilaya hii, nikuombe uendelee kuwatumikia wananchi wetu kwa kasi hii hii uliyoanza nayo.
” Niwaombe pia ndugu zangu wa Ikungi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na muende kuwachagua viongozi ambao ni waadilifu na wenye kuichukia rushwa, msichague viongozi mafisadi, chagueni watu safi watakaoweza kuwatumikia bila kujali itikadi zenu,” amesema Mzee Mtongea.
Kwa upande wake DC Mpogolo ameahidi kuendelea kusimamia miradi ya Serikali kwa uadilifu pamoja na kuwatumikia wananchi hawa ambao walimuamini Rais Dk Magufuli na kumpa kura.
DC Mpogolo amesema atahakikisha wananchi wa Ikungi wananufaika na miradi ambayo imezinduliwa ndani ya Wilaya hiyo ili waweze kuona kazi kubwa ambayo Serikali inaifanya katika kuwahudumia.
” Miradi hii imegharimu Fedha nyingi upo ujenzi wa madarasa mawili ambayo yanaakisi Sera ya Elimu bure inayosimamiwa na Rais wetu kipenzi, mradi wa Maji kama sehemu ya kampeni yetu ya kumtua Mama ndoo kichwani, yote hiyo ni katika kuwatumikia nyinyi wananchi wetu na zaidi kutimiza ahadi ya Rais aliyoitoa kwenu mwaka 2015.