Serikali imesema itaendelea kulinda viwanda vya kuzalisha maziwa nchini ili kukuza soko la ndani na kuhakikisha viwanda hivyo vinazidi kujiimarisha kibiashara kwa kuvipa msamaha wa tozo mbalimbali na kuongeza tozo kwa bidhaa ya namna hiyo inayotoka nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo (20.08.2019) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina jijini Dodoma kwenye kikao cha kutoa taarifa ya tathmini ya sekta ya mifugo ya mwaka 2016/2017 hadi 2031/2032 kwa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, mifugo na Maji ili kujionea namna sekta hiyo inavyochangia ukuaji wa pato la taifa.
“Nataka niseme tuliamua kwa nia njema kupandisha tozo za maziwa kutoka nje kutoka Shilingi 150 hadi Shilingi 2,000 kwa nia ya kuwalinda wazalishaji wa ndani, wizara tukafanya hivyo ili kuona wazalishaji wetu wanavyofanya kazi, sasa hivi kampuni za ndani kila wanachozalisha kwa siku kinanunuliwa chote kutokana na kwamba waliokuwa wakiagiza maziwa kutoka nje waliyo wengi wameshindwa.” Amesema Waziri Mpina.
Akizungumzia kuhusu chanjo za mifugo ili kuhakikisha inakuwa na afya bora na kutoa matokeo mazuri yakiwemo ya upatikanaji wa maziwa, Waziri Mpina amesema serikali itaendelea kuhakikisha inazalisha chanjo za kutosha na kwamba haitaiachia sekta binafsi kuendelea kuzalisha chanjo hizo ili iziweze kupatikana kwa bei nafuu na zenye ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mahmoud Mgimwa amesema Mpango Kabambe wa Mifugo nchini (TLMP) wa mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 uliozinduliwa na wizara hiyo, ukifanikiwa utakuwa na faida kwa wafugaji huku akitaka uwepo mkakati wa upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kama ulivyokusudiwa bila kutegemea wafadhili.
“Ni vyema sasa ikafika wakati serikali ikajielekeza kupanga bajeti ambayo inawiana na mipango tunayoipanga ili mipango hiyo iweze kutekelezwa isije ikatokea moja ya nchi jirani ikanufaika na mipango hiyo kutokana na sisi kushindwa kutekeleza na wao wakachukua wazo wakalifanyia kazi.” Amesema Mhe. Mgimwa
Kikao cha kutoa taarifa ya tathmini ya sekta ya mifugo na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mifugo nchini (TLMP) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel.