NA MWAMVUA MWINYI, KEREGE
VIKUNDI vya Ujasiriamali vya vijana, wanawake ndani ya Kata ya Kerege wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, vimepata mkopo wa sh.milioni 67 kutoka halmashauri ya Bagamoyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Diwani wa kata hiyo Said Ngatipura alisema ,mikopo hiyo imetokana na asilimia kumi ya halmashauri hiyo ambayo ni utekelezaji wa agizo la serikali kwa halmashauri zote nchini kupitia makusanyo yake ya ndani ya kuvikopesha vikundi mikopo isiyokuwa na riba.
“Vikundi hivyo vipatavyo 12 vimepatiwa fedha hizo kulingana na maombi na kiasi cha fedha, huku akieleza kwamba vikundi hivyo vinaendelea na marejesho.
“Kati ya vikundi hivyo vya wanawake vilivyopatiwa mikopo ni 6 kikiwemo cha Tumaini Kilemela ambacho kimerejesha vizuri na kukopa tena, katika mikopo hiyo vikundi vya wanawake vimekopeshwa shilingi milioni 39.5 wakati vijana wakipata mkopo wa sh. milioni 28 ” alisema Ngatipura.
Alifafanua, Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Mwambao Shumina Sharifu, ametafuta wafadhili waliowezesha kuchimba visima viwili vya maji safi, kimoja kipo shule ya msingi Kerege na kingine shule ya Mapinga.
Akizungumzia sekta ya elimu, Ngatipula alisema kuwa Kata ina shule moja ya sekondari yenye kidato cha kwanza mpaka cha nne na wanafunzi 1,105, kati yao wavulana 540, wasichana 565 ikiwa na walimu 75.
Nae Mbunge wa jimbo hilo ,alhaj Shukuru Kawambwa,alibainisha mfuko wa jimbo umeunga mkono juhudi za wananchi katika umaliziaji wa vyumba vya madarasa sekondari ya Kerege, jengo la utawala, vyoo shule ya msingi Mapinga, ununuzi wa bati ofisi ya Kitongoji cha Amani na mifuko 100 ujenzi wa vyumba vya madarasa.