……….
Na Munir Shemweta, WANMM SIKONGE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameiagiza idara ya ardhi katika halmashauri ya Sikonge mkoani Tabora kuhakikisha inawafikisha kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi katika wilaya hiyo wanaodaiwa kiasi cha takriban milioni 150.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo tarehe 15 Agosti 2019 katika halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi sambamba na kukagua masiajala ya ardhi na mifumo ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kielektroniki mkoani Tabora.
Dkt Mabula alishangazwa na idara ya ardhi katika halmashauri hiyo kushindwa kuwafikisha wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba wakati sheria inaelekeza baada ya siku kumi na nne mdaiwa asipotii wito afikishwe kwenye Baraza.
Alisema, katika halmashauri ya Sikonge kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi ambao kwa mara ya mwisho walilipa kodi ya ardhi mwaka 2000 lakini idara ya ardhi imeshindwa kuwadai ama kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria jambo alilolieleza kuwa halikubaliki.
Kaimu Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Martin Ukongo alieleza kuwa ofisi yake tayari ilishasambaza ilani 105 kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi kuanzia januari hadi machi 2019 lakini baadhi yake pamoja na kushindwa kulipa hawajafikishwa kwenye Baraza la Ardhi jambo lililomfanya Naibu Waziri kuagiza hatua za kuwafikisha kwenye Baraza zifanyike.
Dkt Mabula pia ameigiza halmashauri ya wilaya ya Sikonge kupitia idara ya ardhi kuhakikisha inapima mashamba yote yaliyopo katika halmashauri hiyo na kueleza kuwa kutopimwa kwa mashamba hayo kunatoa fursa kwa wamiliki wake kutolipa kodi ya ardhi.
‘’Sikonge mna mashamba hayajapimwa wakati ni ya wafanyabiashara wakubwa hapa wanakwepa kulipa kodi why hamjawapimia na kuwapatia hati ili walipe kodi?’’ Alihoji Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami alisema kuwa Wizara yake kwa sasa imeimarisha mfumo wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kurahisisha ukadiriaji na kufanya malipo kupitia kupitia simu ya mkonini jambo linalowarahisishia wamiliki kuepukana na usumbufu wa kufika ofisi za ardhi kwa ajili ya malipo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019 wilaya hiyo ilifanikiwa kukusanya kodi ya pango la ardhi shilingi milioni 29,127,334.50 sawa na asilimia 87.55 wakati lengo ilikuwa kukusanya milioni 33.2. Hata hivyo Magiri alisema wilaya yake imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kama vile kutoa matangazo na kuelimisha jamii kupitia mikutano umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Sikonge Joseph Kakunda alimpongeza Naibu Waziri Dkt Mabula kwa uamuzi wake wa kufanya ziara katika wilaya hiyo na kueleza kuwa huyo ni Waziri wa Ardhi wa kwanza kuitembelea wilaya hiyo toka ianzishwe.
Hata hivyo, Kakunda alimueleza Dkt Mabula kuwa wilaya ya Sikonge ni wilaya iliyoko nyuma katika suala la Mapango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kuomba Wizara ya Ardhi kuipa kipaumbele katika upimaji ili kuepusha migogoro ya ardhi hasa ile ya wakulima na wafugaji.