NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo amewaasa ,wamiliki wa viwanda kutengeneza bidhaa ambazo zitapata soko kwenye nchi za jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika SADC ili kuinua pato la wananchi na nchi kwa ujumla.
Nchi za SADC zina wanachama 16 ambazo zina wananchi milioni 350 hivyo endapo vitafanikiwa kulipata soko hilo hakika watapata mafanikio makubwa kwa kuongeza kipato cha wananchi na nchi kwa ujumla.
Ndikilo aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kuweka jiwe la msingi ya ujenzi wa viwanda vya Lake Steel and Allied Ltd ikiwa ni ziara yake ya kuweka mawe ya msingi kwenye viwanda 13 vipya.
Aliwapongeza kwa kuitikia wito wa serikali ya awamu ya tano chini ya Dk John Magufuli ya kuhimiza ujenzi wa viwanda ili kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati.
“Viwanda hivyo vinapaswa kutumia mkutano wa viongozi wa nchi hizo kwa kutangaza bidhaa zao kwani endapo watalipata soko hilo watakuwa wafanyabiashara kubwa”alibainisha.
Nae ofisa mtendaji mkuu wa Lake Group Ally Awadhi alisema kuwa lengo kuu la kuanzisha viwanda hivyo ni kuongeza ajira pia kuunga mkono serikali.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani ,Ramadhan Maneno alisema ,ujenzi huo unasidia kupunguza changamoto za ajira kama sera ya chama inavyosema.
Maneno alisema, sera ya chama inahimiza uanzishwaji wa viwanda na kuongeza ajira hasa kwa vijana hivyo hiyo ni utekelezaji wa ilani.
Kwa upande wake,Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama , alisema kikubwa wao kama Wilaya walichokifanya ni kutenga maeneo ya viwanda na uwekezaji mwingine hivyo kuwaondolea usumbufu wawekezaji.
Viwanda vilivyowekewa mawe ya msingi kamapuni hiyo ni cha mabomba makubwa ya maji, mitungi ya gesi cha kwanza hapa nchini na kiwanda cha bidhaa za chuma.