Mabalozi wa Tanzania wakipanda treni ya kisasa baada ya kutembelea mradi huo jana na kuweza kujiona mradi huo ukiendelea
Mabalozi wa Tanzania wakiwa ndani ya Treni ya kisasa baada ya kutembelea mradi wa Reli ya kisasa unaoendelea na kujiona ujenzi huo
Mabalozi wa Tanzania 42 waliotembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa ya Standard Gauge unaoendelea, wakipata picha ya pamoja
Ujenzi wa Mataluma yatakayotumika katika ujenzi wa Reli ya kisasa yakiwa yanatengenezwa na kuzalishwa na kiwanda cha kutengenezea mataluma hayo katika eneo la Soga nje kidogo na jiji la Dar es Salaam.
****************
NA EMMANUEL MBATILO
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw.Masanja Kadogosa amewataka mabalozi wa Tanzania kushirikiana na shirika hilo ili kuleta maendeleo ya miradi inayoendelea hapa nchini na pia kulitangaza taifa kwa ujumla.
Akizungumza na Mabalozi hao waliotembelea mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge(SGR) unaoendelea, Bw.Kadogosa amesema kuwa mpaka sasa ujenzi umefika asilimia 60.4 hivyo amewashukuru mabalozi waliokuja kuangalia mradi wa kimkakati kwani kutawawezesha kulitangaza taifa kwa mazuri yanayoendelea.
“Kama tunaweza kutekeleza miradi hii kwa pesa yetu, watu wa nje watatuheshimu kwa hiyo uwekezaji mkubwa kama huu unawagusa wawekezaji wa nje hivyo sisi tunawashukuru mabalozi kuja kuangalia miradi hii hivyo tunaamini watakaporudi huko watawaelezea watu wa huko kuhusu miradi hii walioyoiona kwa ukubwa wake”. Amesema Bw.Kadogosa.
Aidha,Bw.Kadogosa amesema kuwa gharama za kutengeneza fensi katika ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ni dola bilioni 1.2 kujumlisha na kodi na kutoka Morogoro kwenda Makupola Singida ni dola bilioni 1.9 pamoja na kodi hivyo jumla ya gharama zitakazotumika ni takribani bilioni 3.1.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Swedeni Mh.Wilibrod Slaa amewataka watanzania kujivuna kwa kumpata Rais mwenye kufanya maamuzi kwani wameona miradi mingi ikifanyika hapa nchini hata nchi zilizoendelea wamekuwa wakifanya uwekezaji na kulipa kodi ambazo zinasaidia kuibua miradi mbalimbali.