Home Mchanganyiko Hospitali ya Mloganzila yazindua Baraza la Kwanza la Wafanyakazi

Hospitali ya Mloganzila yazindua Baraza la Kwanza la Wafanyakazi

0

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Charles Majinge akizungumza katika uzinduzi wa Baraza la kwanza la Wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila uliofanyika leo.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la MNH-Mloganzila wakimsikiliza Pro. Majinge wakati wa uzinduzi wa baraza hilo lenye wajumbe 115.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Mloganzila wakiimba wimbo maarufu wa mshikamano (solidarity forever) katika mkutano huo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Charles Majinge (wa pili kutoka kushoto) akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa baraza la wafanyakazi la Hospitali ya Mloganzila, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Prof. Lawrence Museru, wa kwanza kulia ni Katibu Msaidizi wa baraza Bi. Neema Njau akifuatiwa na katibu wa baraza Bw. Nicholaus Mshana.

Prof. Charles Majinge (katikati) akimkabidhi mkataba wa Baraza la Wafanyakazi, Mwenyekiti wa baraza Prof. Lawrence Museru, kulia ni katibu wa baraza Bw. Nicholaus Mshana akishuhudia makabidhiano hayo.

Prof. Charles Majinge (aliyevaa tai , kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Hospitali ya Muhimbili- Mloganzila mara baada ya uzinduzi wa baraza hilo.

……………………………………………………

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Charles Majinge amelitaka Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila kusimamia utekelezaji wa dhamira ya kuhudumia wagonjwa kwa lengo la kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zikiwemo rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na mali za Umma.

Prof. Majinge ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati akizindua Baraza la Kwanza la Wafanyakazi la Muhimbili-Mloganzila.

Amesema baraza la wafanyakazi halina budi kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wake kulingana na sheria na taratibu zilizowekwa, kudumisha utawala bora na kulinda nidhamu sehemu za kazi pamoja na kuondoa aina zote za uonevu au ubaguzi miongoni mwa watumishi.

Pia amewasihi kuhakikisha fedha za serikali zinatumika vizuri kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 2001 na sheria ya ununuzi ya mwaka 2004 kwani utaratibu huu utapelekea matumizi mazuri ya fedha za serikali.

“Mnatakiwa kuhakikisha bajeti ya hospitali inatayarishwa kwa umakini mkubwa ikizingatia vipaumbele, hali halisi ya uwezo wa serikali na mahitaji ya hospitali ili kufikia malengo na kuimarisha huduma za kibingwa’’ amesema Prof. Majinge.

Pamoja na mambo mengine Prof.  Majinge amewataka watumishi wa MNH-Mloganzila kutunza vitendea kazi wanavyovitumia katika kutimiza majukumu yao ili kuweka mali na miundombinu ya hospitali kuwa salama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema baraza la wafanyazi ni la kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa MNH-Mloganzila hivyo amelitaka liwe na mwanzo mzuri.

Amefafanua kuwa Hospitali ya Mloganzila hivi sasa ina miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake hivyo jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha inakuwa na vifaa vinavyotakiwa pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi lengo ni kuhakikisha Mloganzila inakuwa sehemu ya Muhimbili pia isipoteze utambulisho wake.