Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mh Deo Ndejembi ,akizungumza na maafisa ugani wakati wa mkutano maalumu na wakulima wa zao hilo ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara nchini (TNBC)
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mh Deo Ndejembi ,akisisitiza jambo kwa maafisa ugani wakati wa mkutano maalumu na wakulima wa zao hilo ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara nchini (TNBC)
……………..
Na.Alex Sonna,Kongwa
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mh Deo Ndejembi ametoa siku saba kwa maafisa ugani wilayani hapo kumletea tathimini ya mpango kazi wao wa namna gani ya kuweza kuwainua wakulima wa Alizeti wilayani hapo katika kufanya kilimo cha biashara.
Amesema zao la Alizeti ni miongoni mwa mazao tegemezi katika kufikia malengo ya Rais Dk John Magufuli aliyoyaweka ya kuhakikisha Tanzania inakua Nchi ya viwanda.
Hayo ameyasema katika mkutano maalumu na wakulima wa zao hilo ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara nchini (TNBC) ambapo DC Ndejembi amesema maafisa ugani hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha wakulima wanabadilika na kuacha kufanya kilimo cha mazoea.
” Tunaweza kuwalaumu wakulima kuwa hawachangamkii fursa na hawabadiliki lakini kiukweli maafisa ugani wetu ndio wamekua changamoto kwetu, hawaendi site kuwapa elimu wakulima, hawatembelei mashamba wao wanakaa tu mpaka wasikie DC ana ziara ndo wanaanza kukimbizana.
” Sasa natoa wiki moja waniletee mpango kazi wao na baada ya hapo nitaanza ziara ya Kata kwa kata kukagua mashamba yao na namna gani wametoa elimu kwa wakulima wetu, hatuwezi kuwa na watu wasiofanya kazi halafu wanalipwa mshahara huko ni kumhujumu Rais Dk John Magufuli na hilo siwezi kukubali likatokea Kongwa,” amesema Ndejembi.
Amesema lazima maafisa ugani hao wawe sehemu ya kuwasaidia wakulima katika kufanya kilimo bora cha kibiashara lakini pia kuona fursa zingine zilizopo kwenye kilimo.
” Haiwezekani tukawa na maafisa ugani wanaofanya kazi Desemba mvua zibapoanza hadi Aprili zinapoisha, je miezi mingine wanafanya nini huku ni kula mshahara wa bure, tutawachukulia hatua wote ambao hawana mpango wa namna gani tunaweza kuongeza mavuno yetu,” amesema DC Ndejembi.
Aidha Mh Ndejembi amewataka wakulima wa Alizeti kubadilika na kuacha kufanya kilimo cha mazoea badala yake wafanye kilimo cha kisasa wakijua kuwa Alizeti ni zao la biashara na viwanda nchini vinategemea pia zao hilo.
” Mimi nimejifunza kuwa Alizeti haiishii tu kwenye mafuta hata mashudu yale yana thamani kubwa sana, haya mashudu mnayoyadharau yanatengeneza hadi breki za gari. Ndugu zangu wakulima badilikeni ili muweze kuondokana na umaskini, kilimo kinalipa hasa hiki chetu cha alizeti,” amesema DC Ndejembi.
Kwa upande wake Meneja wa Uboreshaji wa Mazingira wa Baraza la Biashara nchini (TNBC), William Magehema amesema wao kama Baraza wamelipa kipaumbele zao la Alizeti na kwamba kupitia kikosi kazi chao cha kilimo watahakikisha kilimo cha zao hilo kinakua ni tija kwa wakulima wa Kongwa ili kuongeza idadi ya mafuta nchini ambayo yatasababisha Serikali iache kumaliza Fedha nyingi kuagiza nje ya Nchi lakini kupitia kilimo hicho pia wananchi waweze kufaidika kiuchumi