Mwenyekiti wa BMT bwana Leodger Tenga akifunga mafunzo ya siku tatu ya walimu wa michezo kutoka shule mbalimbali nchini katika ukumbi wa shule ya St Patrick ya jijini Arusha leo.
Mratibu wa michezo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bwana Leonard Thadeo akizungumza kwenye semina ya walimu wa michezo nchini iliyoendeshwa na wataalamu kutoka chuo kikuu cha Tsukuba cha nchini Japan katika ukumbi wa shule ya St Patrick ya jijini Arusha leo.
Mwenyekiti wa BMT bwana leodger Tenga akiwa na wakufunzi kutoka chuo kikuu cha Tsukuba cha nchini Japan mara baada ya kumalizika kwa semina ya siku tatu kwa walimu wa michezo nchini iliyofanyika katika shule ya st patrick ya jijini Arusha.
Mwenyekiti wa BMT akiwa na walimu wa michezo kutoka mikoa mbalimbali nchini walioshiriki mafunzo ya siku tatu ya utawala na mbinu za michezo katika shule ya st patrick ya jijini Arusha leo
Mkuu wa shule ya St Patrick Bi Dinah Patrick (kushoto) akiwa na wakufunzi wa michezo kutoka chuo kikuu cha Tsukuba cha nchini Japan wakimsikiliza Mwenyekiti wa BMT bwana Leodger Tenga wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya walimu wa michezo katika ukumbi wa St Patrick uliopo Sakina jijini Arusha
………………..
Na Mathew Kwembe, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mashindano ya Michezo ya shule za Sekondari za Afrika Mashariki (FEASSA) utakaofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Jumla ya wanamichezo 3500 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, wenyeji Tanzania bara na Zanzibar pamoja na nchi ya Malawi ambayo imealikwa watashiriki michuano hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha Mratibu wa Mashindano hayo bwana Leonard Thadeo amesema kuwa ufunguzi rasmi utafanyika kesho saa 8.00 mchana kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambapo utachezwa mchezo mmoja wa ufunguzi wa mashindano hayo kati ya timu ya soka ya Lindi dhidi ya timu ya St. Mary’s kutoka Uganda.
“Tayari timu nyingi zimekwishawasili, Uganda waliwasili jana, na nimeambiwa timu kutoka Rwanda jana walilala Singida na kwa ujumla maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo yamekamilika,” amesema.
Mratibu huyo ameitaja michezo itakayoshindaniwa kwenye michuano hiyo kuwa ni pamoja na Soka, riadha, netiboli, mpira wa mikono, mpira wa mikapu, vinyoya, raga, mpira wa magongo, mpira wa meza, mpira wa kengele na michezo mingineyo.
Michezo hiyo imepangwa kuchezwa kuanzia kesho tarehe 16 agosti na fainali za michuano hii inatarajiwa kufanyika tarehe 24 agosti, 2019.
Bwana Thadeo amevitaja viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo kuwa ni pamoja na uwanja wa Magereza, Sheikh Amri Abeid, ISM, St. Constantine, TGT na ukumbi wa michezo wa Paloti.
Wakati huo huo semina ya siku tatu kwa walimu wa michezo wa shule mbalimbali nchini iliyokuwa ikifanyika katika ukumbi wa shule ya St Patrick ya jijini Arusha imefungwa rasmi leo na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania bwana Leodger Tenga.
Akizungumza mara baada ya kufunga semina hiyo ambayo iliwahusisha wakufunzi kutoka chuo kikuu cha Tsukuba cha nchini Japan, bwana Tenga amesema kuwa wamefundisha mambo mengi yakiwemo utawala, mbinu za michezo, afya za michezo pamoja na namna wanamichezo wanavyoweza kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya.
Pamoja na kuwashukuru wakufunzi hao, bwana Tenga amesema kuwa kozi za namna hiyo ni vizuri zikafanyika mara kwa mara kwani dunia imebadilika, michezo siyo tu inafanikiwa kwa kutaka, lazima kuhakikisha kuwa kuna mbinu sahihi, vifaa sahihi na wataalamu sahihi wa michezo.
Amesifu kuwepo kwa ushirikiano baina ya chuo kikuu cha Tsukuba na Tanzania katika kuendeleza sekta ya michezo ambapo chimbuko la ushirikiano huo limetokana na mahusiano baina ya Mratibu wa Michezo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bwana Leonard Thadeo ambaye aliwahi kusoma katika chuo kikuu cha Tsukuba cha nchini Japan.
Bwana Tenga amesema kufuatia kuimarika kwa ushirikiano huo wamewaomba wakufunzi hao wawe wanakuja mara kwa mara nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo ya aina kama hiyo kwani mahitaji ya mafunzo bado ni makubwa sana.