Home Mchanganyiko WAZIRI JAFO AWAASA VIJANA KUTUNZA AMANI

WAZIRI JAFO AWAASA VIJANA KUTUNZA AMANI

0

 

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Seleman Jafo,akizungumza katika maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma leo ambapo amewataka vijana hao kutunza amani ya nchini.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Jacqueline Mahon,akitoa taarifa katika maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Vijana,Sanaa,Utamaduni na Michezo,Zanzibar,Amour Hamil Bakari,akizungumza na washiriki katika maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

Msanii wa bongofleva Kala Jeremiah,akitoa burudani pamoja na washiriki katika maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Seleman Jafo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya vijana katika maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma

.WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Seleman Jafo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi katika maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.

Picha na Alex Sonna-Fullshangweblog

………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Mhe.Seleman Jafo amewataka vijana  kutochezea amani ya Nchi na Badala yake wawe Mabalozi Wazuri wa kutunza na kuenzi amani hiyo kwani ni Tunu kwa Taifa la Tanzania.

Waziri Jafo amesema hayo leo  jijini Dodoma katika maadhimisho ya siku ya vijana duniani ambapo amesema amani iliyoasisiwa na Marais wa Tanganyika na Zanzibar ni vigumu kuirejesha ikipotea hivyo vijana  ni nguzo Muhimu wa Kuitunza amani hiyo.

“Waasisi wa Taifa letu ,Julius Kambarage Nyerere na Aman Karume walipambana sana na walitumia gharama kubwa kuhakikisha amani ya nchi yetu inapatikana na tukajipatia Uhuru ,kilichobaki ni kirahisi sana ni kuiendeleza ,kuienzi na kuitunza amani ya Nchi Yetu  kwani ikipotea kuirudisha ni vigumu sana ,na wenye wajibu na nguvu kubwa wa kuinza ni ninyi vijana “amesema Jafo.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewataka vijana waliopewa nafasi  za Madaraka kufanya kazi na kuacha maigizo ili waache historia ya Taifa la Tanzania.

Waziri Jafo amesema ni vyema kwa vijana waliopewa dhamana ya kuliongoza taifa  kuwajibika vyema kuwahudumia Wananchi .

Pia amewataka  kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na Halmashauri ambapo amedai kwa sasa kina mama ndio wamekuwa wakichangamkia fursa hiyo.

 “Igeni mfano wangu mimi simwangushi Rais,bajeti ya nchi zaidi ya asilimia 20 inatoka kwangu,vijana mkipewa nafasi fanyeni kazi.Usikubali ukiwa kama kijana lazima uache alama ili wakukumbuke,kijana sio sifa kukaa kiti kirefu halafu unasema kunyweni mpaka mikono idondoke, acha alama wekeni mifano kwa watu wengine,”amesema .

“Vijana acheni maigizo  fanyeni kazi ya kuwasaidia Watanzania fanya kazi kwa ajili ya kuwahudumia watu,fanya kazi yako itangazike,tukifanya maigizo hatuwezi kulisaidia Taifa letu.Niwaombe vijana wenzangu tupambane,”amesema.

Jafo amesema vijana ambao wamepewa fursa wasivunje  matumaini ya vijana wenzao.

Amewataka vijana kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa katika Halmashauri mbalimbali nchini huku akidai kwamba wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi.

“Bado ni changamoto,lazima tuangalie namna ya kurejesha mikopo wengi wanaorejesha ni kina mama,vijana wanaokopa kurejesha ni shida,”alisema Jafo.

Jafo amewataka vijana kulima kilimo cha kisasa kwani kimekuwa na faida kubwa ambapo alidai ekari moja ikipandwa vizuri inaweza kutoa mazao mengi.

“Ukiamua kufuga kuku wa mayai 10,000 ambao kila siku wanatoa trei 300 kwa shilingi 7000 ina maana kila siku wana uwezo wa kupata milioni moja.Vijana naomba niwaambie badilishaneni mawazo,wekezeni katika ujasiriamali,”alisema.

Aidha,Jafo aliwataka vijana ambao watajadiliana katika kikao hicho kufanya tathmini ya yale watakayokubaliana nayo na kisha wanayapeleke Serikalini.

“Tumepata fursa ya kukutana bahati nzuri kutoka katika mikoa yote nawaomba mfanye tathmini ya mambo yote na yale mtakayokubaliana yaleteni Serikalilini na tutayafanyia kazi.

“Zamani kulikuwa na kauli mbiu vijana ni taifa la kesho kauli hiyo tumeitoa na kwa sasa vijana ni taifa la leo,vijana sasa mnaweza kupewa fursa na mkapewa nafasi mkazitendea haki.

Jafo amesema wana kila sababu ya kujadiliana kuhusu elimu kwani imekuwa ni daraja la kuweza kufikia mafanikio.

“Kumbukeni tuna kila sabbau ya kujadili ajenga ya elimu, tuna kila sababu ya kuboresha elimu yetu bila elimu vijana wa sasa hatuwezi kupasua tuna kila sababu ya kuitafakari elimu yetu.Niwaombe sana lazima vijana wa kitanzania tujikite katika elimu.

Aidha,Jafo amewataka vijana kujitambua kwa kuhakikisha wanakuwa na uzalendo  wa kununua bidhaa zinazozalishwa na vijana.

“Tuna agenda kubwa tupambane na adui wa roho mbaya kuna vijana wengine wana roho mbaya wapo kuwakwamisha kwanza tupendane,bidhaa hizo zote kama tutanunua tutaenda mbali kwani vijana ni timu kubwa,”amesema.

Kwa Upande wake,Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Vijana,Sanaa,Utamaduni na Michezo,Zanzibar,Amour Hamil Bakari,amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kuchukua juhudi kuhakikisha vijana wanapata kazi pamoja na kufanya kazi zenye staha. 

“Serikali zinaendelea kuchukua juhudi kuhakikisha vijana wetu wanapata kazi zenye staha pamoja na changamoto ya ajira.Niwakumbushe vijana kuendelea kulinda amani iliyopo, suala la kudumisha muungano wetu hili halina mjadala na sisi tutaendelea kuwakumbusha vijana kuhakikisha wanalinda muungano kwa nguvu zote,”amesema.

Naye,Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA)Jacqueline Mahon amesema vijana  wanatakiwa kusaidiwa kwenye mambo mbalimbali.

Pia amesema elimu ni Msingi  wa Maendeleo endelevu kwa vijana ndio maana maadhimisho ya vijana duniani mwaka 2019 imelenga zaidi kuimarisha elimu kwa vijana na UNFPA imekuwa ikijikita zaidi kutatua changamoto mbalimbali za vijana ikiwa ni pamoja na changamoto ya elimu na Ajira Kwa Vijana.

Hivyo  Madam Mahon amesema UNFPA ina mkakati Kabambe wa kuwawezesha vijana kwa kushirikiana na Mashirika mbalimbali ya Tanzania na ya Kimataifa huku akizungumzia mkutano Mkubwa wa Vijana utakaofanyika jijini Nairobi nchini Kenya na kuwaasa vijana kujitokeza kwa wingi kwani vijana ni chachu muhimu kwa Maendeleo ya nchi.

Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya vijana,Maadam Sophia Mbeyela ameshukuru serikali pamoja na asasi za kiraia kwa kujali vijana wa rika zote na aina zote wakiwemo wenye ulemavu na kusema kuwa wao kama vijana wenye ulemavu hawaachwi nyuma kwani ulemavu si ugonjwa.

Awali Afisa Maendeleo ya Jamii ,Idara kuu ya vijana  jiji la Dodoma Mfungo Daniel Manyama ambaye alikuwa mwakilishi wa Afisa vijana Mkoa wa Dodoma , amewaasa vijana kuchangamkia Fursa ya Zao la Zabibu pia  kuunga mkono vijana

wenzao kununua zao hilo ili kuinua uchumi wa vijana huku Mkuu wa Chuo Mipango na Maendeleo ya Vijijini ,Prof.Hozen Mayaya akiwataka vijana kuwa na Fikra pevu.

Siku ya Umoja wa Mataifa ya Vijana imeratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa Tanzania UN na kuongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu UNFPA ,kwa kushirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania UNICEF,UNESCO,UNIC na ILO pamoja na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mkoa wa Dodoma na Asasi zisizo za Kiserikali.