Viongozi wa Skauti Mkoa wa Katavi wakiwa katika Ukumbi wa manispaa ya Mpanda
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera akiwa amepokea Tuzo ya Mkoa wa Katavi kushiriki katika Jamboree ya Skauti Zanzibar
Viongozi wa skauti wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Katavi
…………………..
Na Mwandish wetu Katavi
Wazazi mkoani Katavi wametakiwa kuwaruhusu watoto wao kujiunga na Chama cha Skauti Tanzania kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia vijana kujifunza mambo mbalimbali ya ukakamavu pamoja na kuepuka tabia hatarishi
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Skauti mkoa wa Katavi bwana Clavery Jonas mara baada ya kuwasilisha tuzo ya kushiriki kongamano la Skauti Zanzibar kwa Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera
Bwana Clavery alisema mafunzo ya skauti yanawaandaa vijana kuwa raia wema, na kutokufanya vitendo vya uovu kama kuchoma shule na kupiga walimu
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo Mkuu wa Mkoa wa Katavi bwana Juma Homera amewataka viongozi wa wilaya kuwapa ushirikiano wa kutosha skauti
“Skauti inasaidia watoto kujenga ukakamavu hivyo niwaombe wakuu wote wa wilaya na wakurugenzi msisite kushirikiana nao” alisema Homera
Aidha viongozi wengine wa skauti wamewataka wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuondoa mtazamo hasi kwa skauti
Bi. Diana Philipo ni Kamishna wa Skauti wilaya ya Tanganyika amewataka wazazi kuwatoa watoto wao wa kike kujiunga na skauti kwani mafunzo hayo yanamjengea mtoto maadili mema
Kwa upande wake mwalimu John Ndumbaru ambaye ni Naibu Kamishna wa Skauti mkoa wa Katavi amewataka walimu kushiriki katika makongamano mbalimbali ya skauti yanayofanyika mkoani Katavi ili kuwajengea utayari
“Skauti ni sawa na askari wa kisiri siri, hivyo tukiwa na maskauti wengi tutaimarisha ulinzi katika mkoa wetu” alisema mwalimu Ndumbaru
Naye naibu Kamishna wa Skauti katika Manispaa ya Mpanda bwana Stanslaus Boniface amewataka wazazi kuwatoa watoto wao kwa ajili ya kushirikiana nao kwani skauti ni mali ya serikali na haihusiani na Chama chochote cha siasa