Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe akiongoza kikao cha pamoja katika ya Wataalam kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA pamoja na Idara ya Usalama wa Chakula walipokuwa wakiteta na Ugeni kutoka Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ukiongozwa na Bi. Miriam Van Den Bergh na Riaz Lodhi
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe akiongoza kikao hicho kushoto kwake ni Eng. Imani Zobonaliba na Bwana Ally Mohamed kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
Ugeni kutoka Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) kutoka kushoto ni Bi. Nima Sitta Mwakilishai wa WFP Ofisi ya Dodoma, Bi. Miriam Van Den Bergh Msimamizi Mkuu wa Ununuzi wa Mazao ya Chakula Afrika, Riaz Lodhi, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Mnyororo wa Thamani wa Mazao Tanzania na wa mwisho ni Bi. Wambui Mbugua Msimamizi wa Manunuzi ya Mazao Kenya
…………………….
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Eng. Mathew Mtigumwe amewahamasisha Wakulima wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa kuanza kulima mtama mweupe kwa wingi kwani tayari kuna soko la uhakika kutoka kwa Shirika la Mpango la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).
Eng. Mtigumwe ameyasema hayo wakati wa mazungumzo yake na ugeni kutoka Ofisi ya WFP Kanda ya Afrika, ugeni uliotokea Jijini, Nairobi nchini, Kenya ukiongozwa na Bi. Miriam Van De Bergh ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa Ununuzi wa Mazao ya Chakula Afrika.
Eng. Mtigumwe amesema ugeni huo umemuhakikishia kuwa Wakulima wa mahindi wa Tanzania kuwa wataendelea kunufaika na uwepo wa Shirika hilo lakini pia wametoa fursa ya kununua mtama mweupe kutoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuwa hali ya hewa inaruhusu zao hilo kulimwa lakini pia itakuwa rahisi kwa Shirika hilo kusafirisha shehena ya zao hilo baada ya kuvunwa.
Akiongelea hali ilivyo ya fursa mpya ya kununua mtama mweupe Bwana Riaz Lodhi, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Mnyororo wa Thamani wa Mazao Tanzania amesema WFP imeichagua Tanzania kuwa sehemu ya eneo la kununua mtama mweupe kwa kuzingatia vigezo vingi kama; hali ya hewa, mahusianao ya muda mrefu ya kibiashara pamoja na nguvu kazi iliyopo.
Bwana Liaz ameongeza kuwa mwaka jana pekee WFP ilinunua kiasi cha tani elfu 80 (80,000) za mtama mweupe kutoka nchi za jirani na kusafirisha shehena hiyo hadi Sudan Kusini.
“Tumeona ni vyema tuilete fursa hii kwa Tanzania na Katibu Mkuu naomba utufikishie ujumbe huu kwa Wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kuchangamkia fursa hii ya kulima mtama mweupe, sisi tutaununua kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA na kupeleka kwenye maeneo yenye uhitaji kama Sudani Kusini”. Amekaririwa Bwana Liaz.
Kwa upende wake Eng. Mtigumwe amesema kwa kuanzia Wizara itawahamasisha Wakulima kuanza kulima zao hilo kwa wingi lakini pia atatoa maelekezo kwa Taasisi ya Utafiti ya Kilimo (TARI – Ukiliguru) kutoa elimu na aina bora za mbegu za mtama mweupe kwa ajili ya kuwapa Wakulima.
“Nitawaita Taasisi yetu ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili tuweke mazingira mazuri ya kuchangamkia fursa hii ya kulima zao la mtama mweupe kwa Wakulima wetu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa”. Amekaririwa Katibu Mkuu, Eng. Mtigumwe.