Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akipokea taarifa kutoka kwa Msimamizi wa Ujenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Suleiman Salmin kuhusu miradi ya ujenzi inayotekelezwa na mfuko huo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi hiyo.
Msimamizi wa Ujenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Suleiman Salmin (kushoto) akielezea jambo kuhusu hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa jengo la hoteli ya nyota tano (5) inayojengwa na Mfuko huo, Jijini Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelezo kwa watendaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipotembelea kwa lengo la kukagua na kujionea hatua za awali zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitazama jengo mmoja wapo linalojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakati ziara yake ya kukagua na kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
……………….
Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameagiza watendaji wa Mifuko ya hifadhi ya Jamii yaani Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa wabunifu katika kuwekeza kwenye vitega uchumi vyenye kuleta tija na inayochochea maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake Jijini Mwanza alipokuwa akikagua Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii ili kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji.
Alieleza kuwa kuwekeza katika miradi yenye tija ni jambo muhimu kwa kuwa miradi hiyo italeta maendeleo endelevu yatakayochangia katika ukuaji wa pato la taifa na ustawi wa mkoa huo.
“Mwanza ni miongoni mwa Mikoa yenye fursa nyingi za kibiashara kutokana na sehemu kubwa ya mkoa huo kuzungukwa na ziwa viktoria, hivyo kurahisisha ukanda huo kufikiwa kwa urahisi na soko la Afrika Mashariki,” alisema Mhagama.
Alifafanua kuwa ubunifu katika kutekeleza shughuli za mifuko ni pamoja na kutafuta masoko ya vitenga uchumi ya miradi hiyo kwa kuangalia fursa zilizopo kwenye kanda ya ziwa.
Aliongeza kuwa fursa ni pamoja na ujenzi wa daraja la Busisi litakalopita ziwa viktoria, Mbuga ya Wanyama ya Burigi pamoja na shughuli za uchimbaji madini zilizopo katika mkoa huo.
Katika Ziara hiyo Waziri Mhagama aliweza kutembelea linapojengwa Soko la Madini katika Jengo la Kibiashara la Rock City Mall. Pia alitembelea jengo la PSSSF Mwanza na alipata fursa ya kukagua shughuli za uwekezaji katika jengo hilo zinazoendeshwa na wawekezaji wazawa katika Hoteli ya Gold Crest.