Home Mchanganyiko TERRAT WALIA NA UMEME 

TERRAT WALIA NA UMEME 

0

Baadhi ya viongozi wa CCM wa  matawi, Kata na Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wakijiandaa kuingia ndani ya kikao cha mikakati ya ushindi wa uchaguzi wa serikali za mitaa na kumpongeza Rais John Magufuli kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati ya maendeleo.
Diwani  wa kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Ole Materi akizungumza juu ya viongozi kutouza ardhi. 
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Daniel Ole Materi akizungumza juu ya mikakati ya ushindi wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
*****************
WAKAZI wa Kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameiomba Serikali kufanikisha awamu ya tatu ya mpango wa usambazaji wa nishati ya umeme vijijini (REA III) ili visima na viwanda vidogo viweze kukamilika na kuwanufaisha kiuchumi. 
Wananchi hao waliyasema hayo wakizungumza kwenye kijiji cha Terrat katika kikao cha kupanga  mikakati ya ushindi wa uchaguzi wa serikali za mitaa na kumpongeza Rais John Magufuli kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya kimkakati. 
Katika kikao hicho kilichohusisha viongozi wa CCM wa kata tatu za Komolo, Terrat na Oljoro namba tano za Tarafa ya Terrat, walidai kuwa nishati ya umeme ikifika kwenye eneo hilo itawanufaisha zaidi tofauti na sasa wanapotumia nishati ya umeme wa jua (Sola) na majenereta. 
Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi  alisema katika mpango wa visima 20 vya wilaya hiyo, kata hiyo ilifanikiwa kupata visima viwili ila wanashindwa kuviendesha kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme. 
“Rais John Magufuli kupitia ilani ya CCM anatekeleza suala zima la kumtua mwanamke ndoo kichwani lakini tunashidwa kutekeleza hilo kwa ukosefu wa nishati ya umeme ila tuna matarajio utafika na maji yatakuwepo kwa wingi,” alisema Ole Materi. 
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa wa wilaya ya Simanjiro Daniel Ole Materi alisema kiwanda cha maziwa kimeshidwa kufanya kazi kutokana na kutowepo kwa nishati ya umeme. 
“Gharama za nishati ya umeme wa jua na jenereta ni ghali mno katika kuendesha viwanda, tunaiomba serikali ifanikishe hili suala la umeme wa Rea kwani ni hitaji kubwa kwa jamii,” alisema Ole Materi. 
Hata hivyo, ofisa Tarafa ya Terrat, Lekshon Kiruswa alisema suala la mradi wa Rea awamu ya tatu kwenye eneo hilo unaendelea vizuri kwani vijiji vingi katika tarafa hiyo vimepata umeme. 
Kiruswa alisema kata za Oljoro namba tano na Komolo zimeshapata nishati  ya umeme na hivi sasa unaelekea kijiji cha Nadonjukin kisha utaingia kata ya Terrat na kuendelea kusambazwa katika vijiji vya eneo hilo. 
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na nishati ya umeme huu wa Rea na kutokana na kasi kubwa inavyokwenda utekelezaji wake utafanikiwa. 
Mkazi wa kijiji cha Terrat Jacob Laizer alisema endapo nishati ya umeme ingefika katika eneo hilo hivi sasa kungekuwa na maendeleo makubwa mno. 
“Kuna wafugaji wana uwezo wa kufungua viwanda vidogo ili kumuunga mkono Rais John Magufuli katika dhana ya Tanzania ya viwanda ila wanashindwa kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme,” alisema Laizer.