NJOMBE
Chama cha wafugaji wa ng’ombe wa Maziwa mkoani Njombe NJORIFA kimeitaka serikali kuvunja uongozi wa kiwanda cha maziwa akiwemo meneja wa kiwanda hicho kwa kushindwa kuendesha kiwanda hicho ipasavyo hatua ambayo inafifisha maendeleo ya sekta ya maziwa nchini.
Wakifafanua sababu ya kuomba kutimuliwa kazi safu ya utawala wa kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa mfumo wa hisa na watu mbalimbali wakiwemo wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wamesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu kiwanda kimeshindwa kulipa wafugaji na kusababisha malimbikizo ya zaidi ya mil 100 jambo ambalo linawafanya waishi maisha magumu na kulazimika kuuza mashamba na miti ili kukimu familia na mahitaji ya shule kwa watoto wao.
Wafugaji hao akiwemo Octavina Kiwule,Benitho Mgohele na Octatusi Ngole wamesema wanashangazwa na kitendo cha kiwanda hicho kushindwa kulipa fedha za maziwa kwa wafugaji ili hali kimekuwa kikichukua kila uchwao maziwa kwa wafugaji na kuyauza bila ya kufanya malipo kwa wazalishaji kwa zaidi ya awamu nne hadi tano hatua ambayo imekiuka makubaliano ya kimkataba walisainiana.
Kutokana na hali hiyo wameomba mkuu wa mkoa kuvunja uongozi wa kiwanda ili kunusuru sekta ya maziwa mkoani Njombe kwa kuwa uongozi huo umepoteza imani kwa wafugaji kwani kumekuwa na upotevu wa fedha za wafugaji kiasi cha zaidi ya mil 48 katika mazingira ya ajabu na kucheleweshwa kwa malipo.
Mzee Walter Mwanyika ni mwenyekti wa NJORIFA anasema maisha ya wafugaji yanazidi kuporomoka kwasababu ya uwezo mdogo wa uongozi hatua ambayo inawafanya kuona ulazima wa mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka kuingilia kati suala hilo ili kunusuru kiwanda na wafugaji kwa kuwakutanisha wamiliki wote watano wakiwanda ikiwemo halmashauri ya mji na wilaya ya Njombe zenye hisa 9.5 kila moja,Roman Katoriki yenye hisa 9.7,waitaliano wenye hisa 16, Njorifa nyenye hisa 20 pamoja na kiwanda chenye 30.
Mtandao hu umefanikiwakuzungumza na uongozi kuthibitisha malalamiko ya wafugaji na kufanikiwa kuongea na meneja rasilimali watu Michael Malangalila ambaye anakanusha madai ya mil 100 na kudai kwamba kiwanda kinadaiwa mil 44 pekee na wakulima hivyo kipo katika mchakato wa kulipa huku akitaja sababu ya utanuzi wa kiwanda kuchangia kusuasua kwa ulipaji wa madeni hayo.