Mkurugenzi wa Kilimo, Chakula na Maliasili wa jumuiya hiyo Domingos Gove akizungumza na waandishi wa habari za mikutano ya SADC inayoendelea jijini kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo.
………………………………………………………..
JUMUIYA ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)imesema ipo kwenye mkakati wa kuanzisha mfuko wa kilimo wa kanda kwa ajili ya kusaidia nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Hayo yamesemwa leo Agosti 11, 2019 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kilimo, Chakula na Maliasili wa jumuiya hiyo Domingos Gove wakati anazungumza na waandishi wa habari za mikutano y SADC inayoendelea jijini.
“Kwa sasa tupo katika mkakati wa kuanzisha mfuko wa kilimo wa pamoja wa kikanda ambao lengo ni kuhakikisha tunasaidiana katika chakula kwa nchi za SADC,” amesema Gove.
Amefafanua katika mkakati huo pia watahakikisha kunakuwa na miundombinu itakayofanikisha nchi wanachama zinajikita kwenye kilimo kwa ajili ya kupata chakula cha kutosha kwa nchi zao.
Mkurugenzi huyo wa Kilimo,Chakula na Maliasili ameongeza kuwa kwenye mfuko huo ambao utaanzishwa kwa nchi za SADC utahakikisha kunakuwa na usambazaji wa mbegu bora zisizo na magonjwa , upatikanaji wa soko kwa malighafi zinazohusika kwenye suala la kilimo.
Pia amesema mikakati mingine ni kuongeza ushindani na uzalishaji wa nafaka pamoja na kuhakikisha kunakuwa na sera ya kulinda usalama wa chakula.
“Tumejipanga kuhakikisha kupitia mfuko huo wa kilimo tunazalisha chakula kwa wingi na pale ambapo nchi mojawapo itakuwa na tatizo la uhaba wa chakula basi tunasaidia kupeleka chakula kutoka kwenye nchi zenye chakula cha ziada,”amesema.
Ameongeza vyakula ambavyo vitazalishwa pamoja na mambo mengine vitazingatia suala la lishe kuhakikisha walaji wanakuwa na afya njema na imara kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo kwa nchi wanachama.
Wakati huo huo jumuiya hiyo imeeleza namna amavyo imejipanga katika kuhakikisha nchi za jumuiya hiyo zinakuwa na miundombinu yenye uhakika.
Ambapo kwenye eneo hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Habari, Matangazo na Machapisho ya Kamati Ndogo ya Kamati Kuu ya SADC Zamarad Kawawa ametumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo Serikali ya Tanzania ilivyoweka mkazi katika ujenzi wa miundombinu.
“Tanzania tuko vizuri, katika eneo hilo, ukienda bandarini, viwanja vya ndege , reli, na barabara kote kumeimarika kwa kiwango kikubwa,”amesema Kawawa ambaye pia nia Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari(MAELEZO).
Mwenyekiti wa Kamati ya Habari, Matangazo na Machapisho ya Kamati Ndogo ya Kamati Kuu ya SADC Zamarad Kawawaakiwa katika mkutano huo kulia ni Barbara Lopi Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano SADC.
Barbara Lopi Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano SADC akizungumza na kutoa ratiba ya mikutano mbalimbali inayoendelea jijini Dar es salaam.
Innocent Mbrundula Ofisa Mawasiliano na Uhusiano SADC akifafanua jambo katika mkutano huo.
Picha zikionesha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifuatilia mkutano huo uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.