…………………
Na.Alex Sonna,Kongwa
Mkuu wa wilaya ya Kongwa iliyopo jijini Dodoma Deogratius Ndejembi amesema wahusika wote waliofanya ubadhilifu wa fedha za ujenzi katika Shule ya Sekondari Kongwa mkoani Dodoma Watazitapika.
Ndejembi amesema hayo Agosti 9,2019 alipofanya ziara shuleni hapo kwa lengo la kuangalia mwenendo wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kongwa mradi huo umegharimu zaidi ya Tsh.Milioni 290 fedha zilizotolewa na Serikali.
Mkuu huyo wa wilaya ametaja miundombinu inayojengwa katika shule hiyo ni pamoja na mabweni mawili ambapo kila moja lilitengewa Tsh.Milioni 75 lakini hayatakamilika kutokana na fedha kuisha,Bwalo lilitengewa milioni 100 lakini nalo pia halitakamilika kutoka na kubaki mifuko ya saruji 40 pekee .
Hata hivyo, amebainisha kuwa kwa upande wa Madarasa yatakamilika kwa milioni 36 huku fedha zilizobaki kwenye akaunti ni milioni 74 pekee ambazo hazitaweza kutosheleza katika ukamilishaji wa miundombinu yote na zilizobaki nje ya akaunti laki moja na nusu pekee.
Mhe.Ndejembi amesema sababu zilizosababisha majengo hayo kutokamilika licha kutengewa fedha nyingi ni kutokana na kutofuata maelekezo ya Serikali ya kutumia Force akaunti ambapo walitangaza tenda hali iliyosababisha ununuzi wa vifaa vya ujenzi kununuliwa kwa bei kubwa tofauti na ilivyo kawaida na ameshangazwa kwa maeneo mengine hapa nchini yamekamilika.
Hivyo Mkuu huyo wa wilaya ameagiza TAKUKURU kufuatilia bei ya Manunuzi ya Bidhaa hizo za Ujenzi ,milioni 74 zilizobaki kwenye akaunti zisitume mpaka uchunguzi ukamilike na wale wote waliohusika katika ubadhilifu huo wanachukuliwa hatua kwa kumdanganya na kumdharau Rais,Waziri wa TAMISEMI pamoja na yeye.